Sunday, 20 May 2018

Waziri Mkuu akerwa utitiri wa tozo zao la Kahawa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya nchini wakutane na wadau wa vyama vya msingi vya zao la kahawa na wapitie upya tozo zilizo kwenye zao hilo.

Amesema tozo nyingi haziko kisheria bali zinawekwa na vyama vya msingi na zimelenga kuwanyonya wakulima badala ya kuwasaidia kuinua vipato vyao.

Ametoa kauli hiyo jana Mei 19, 2018, wakati akizungumza na Warajis Wasaidizi wa Ushirika wa Mikoa 25 na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya 140 zinazolima mazao makuu ya biashara yaani kahawa, chai, tumbaku, pamba na korosho.

Walikuwa kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kujadili namna bora ya kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo alikwishayatoa kwenye ziara zake mikoani.

Tangu mwaka jana, Waziri Mkuu ameshafanya vikao zaidi ya sita na wadau wa pamba, korosho, tumbaku na kahawa nchini ili kubaini namna bora ya kufufua mazao hayo makuu.

Akizungumzia kero ya tozo za mazao kwa wakulima, Waziri Mkuu alisema:

 “Kuna tozo nyingi zinazowekwa na vyama vya msingi na hazina uhalali wowote; tozo nyingine si za vyama vikuu, bali ni za AMCOS tu (vyama vya msingi).”amesema

No comments:

Post a comment