Sunday, 13 May 2018

Waziri Kigwangalla kabidhi magari Halmashauri sita

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dk.Hamisi Kigwangalla amekabidhi magari kwa Halmashauri 6 kwa ajili ya kupambana na vita dhidi ya ujangili.
Magari hayo amewakabidhiwa Wabunge  leo katika ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii  Jijini  Dodoma.
Wabunge waliokabidhiwa magari hayo ni wa  Bunda Vijijini,Boniface Getere ,Itilima,Njalu Silanga ,LongIdo,Dk.Steven Kiruswa,Mbulu Vijijini Flatei Massay,Tanganyika,Moshi Kakoso huku Mbunge wa Ngorongoro,William Ole Nasha yeye hakuweza kufika kutokana na kubanwa na majukumu mengine.
Wabunge hao wamepokea kwa niaba ya Halmashauri hizo.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi magari hayo,Dk.Kigwangalla amesema jumla ya Halmashauri 6 zinatarajiwa kunufaika na magari hayo.
“Tunakabidhi magari ambapo Halmashauri 6 zitanufaika ambayo yanatokana na jitihada za Waheshimiwa Wabunge kutusumbua sana lakini pia utashi wao katika kuunga mkono katika vita dhidi ya  ujangili.
“Lakini pia magari haya yatatusaidia kwenye doria katika maeneo hayo lakini pia ‘kurespond’ haraka kesi za wanyama waharibifu   mfano katika  maeneo kama kule Bunda Vijijini katika vijiji vya Mugumu na Mgeta kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana wa wanyamapori na makazi ya watu.
“Lakini bahati mbaya Halmashauri zinakuwa hazina usafiri wa ‘Kurespond’ haraka kwenda kuwaondoa wale wanyama hivyo tumeona tuwape gari kama kule kwa wahadzabe,Longido tumeona tuwape magari.
“Maeneo kama Itilima hata juzi  nilishuhudia kwa masikitiko makubwa watu wawili wakipoteza

maisha kwa kuvamiwa na Tembo na Tembo hao walihamia kabisa wakaweka kambi na wamemaliza mazao ya wananchi na wamesababisha vifo.
“Tuliona tuzisaidie Halmashauri zetu hivi ili na zenyewe zipate vyombo vya uhakika ili waweze kufika haraka.
Waziri huyo amesema sambamba na makakati huo pia Serikali inakusudia  kujenga madungu kwa ajili ya kuangalia wanyama tokea wakiwa mbali ndani ya hifadhi.
Pia amesema wanatarajia  kuweka uzio wa mizinga ya nyuki ili kuzuia wanyama kama Tembo wasitoke katika maeneo ya hifadhi.
“Wenzetu hawa wa Tanganyika wao wana msitu mzuri wa Tongwe ambao una nyani na tayari tumeishapitisha msitu wa Tongwe uwe hifadhi na utakuwa chini ya Halmashauri hivyo tumeona tuanze kuwajengea uwezo wa usafiri ili waweze kuuendesha.
Dk Kigwangalla ametoa angalizo kwa halmashauri zilizopewa magari kuwa yatumike kwa shughuli za maliasili pekee na sio zingine
“Napenda kutoa angalizo kwa hizi halmashauri zilizopewa haya magari yatumike ipasavyo kuanzia ulinzi wa maliasili uendelezaji wa maliasili na kutoa elimu kwa wananchi na zisitumike kwa shughuli zingine,”
“Naomba suala hili lizingatiwe na tayari tumeishamwelekeza Katibu Mkuu ataandika barua mahususi ambayo itatoa maelekezo mahususi na kama kutakuwa tofauti tunaweza kuchukua hatua ikiwemo kuyachukua magari yetu,”alisema
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Maj. Gen. Gaudence Milanzi amesema wametoa magari hayo kutokana na maelekezo ya Waziri wa Wizara hiyo Dk.Kigwangalla kuwa yatolewe magari katika maeneo ambayo yanauhitaji wa kulinda uhifadhi na wanyamapori.
“Waziri umeelekeza tutoe magari kwa baadhi ya maeneo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kulinda malisili zetu na leo tunawakabidhi hawa Waheshimiwa Wabunge,”alisema
Naye Mbunge wa Mbulu Vijiji, Flatei Massay alimshukuru Waziri kwa kuwapatia magari hayo huku akiahidi kuwa yataenda kutumika kwa mahitaji yaliyokusudiwa

No comments:

Post a Comment