WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa  na Serikali za  Mitaa (TAMISEMI),  Selemani Jafo, ameagiza  kufikia  mwezi Desemba mwaka huu taasisi zote za serikali katika halmashauri ya  jiji la Dodoma zinatakiwa kupata  hati miliki ya maeneo yao.

Aidha,  ametoa muda wa mwezi mmoja kukamilishwa kwa ujenzi wa kituo cha afya cha Hombolo jijini  hapa ambacho kimeonekana kuwa ujenzi wake upo nyuma ikilinganishwa na vituo vingine 208 vinavyokarabatiwa nchini.

Jafo alitoa maagizo hayo juzi mara baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa kituo cha afya Hombolo iliyotolewa na Mganga wa kituo hicho kilichopatiwa fedha kiasi cha Sh. milioni 500 na serikali kwa ajili ya ukarabati.

Katika taarifa hiyo ya ujenzi moja ya changamoto iliyotolewa na Mganga wa kituo hicho,  Dk.Hosea Lotto alisema kituo hicho hakina hati miliki.Dk. Lotto alisema pamoja na majengo ya kituo cha afya Hombolo kuwepo toka mwaka 1968,  lakini mpaka hivi sasa  hawana hati miliki kutoka mamlaka husika.

Kutokana na hali hiyo, Jafo aliagiza hadi kufikia Desemba  mwaka huu jengo hilo liwe tayari limepatiwa hati miliki na kumtaka Mkurugenzi wa jiji kuhakikisha jambo hilo linafanyiwa kazi ipasavyo.

“Haiwezekani toka mwaka 1968 hadi leo hii hamna hati miliki na uongozi upo umekaa tuu halafu leo mnaniambia hamna hati miliki sasa mnataka mimi niwatafutie hiyo hati miliki…sasa kuanzi leo nataka hadi ifikapo mwezi Desemba katika halmashauri ya jiji la Dodoma taasisi zote zikiwemo za elimu na afya, ziwe na hati miliki”

“ Haiwezekani watu wanakuja leo wanapatiwa kiwanja na hati miliki harafu nyinyi jengo lenu halina hati miliki watu wanaweza kuanza kuvamia eneo la kituo kwa kujenga ovyo makazi yao,”alisema Jafo.

Aliuagiza uongozi wa halmashauri ya jiji la Dodoma pamoja na kituo cha afya kuhakikisha kuwa ujenzi unakamilika ifikapo Juni 30 mwaka huu na siyo vinginevyo.

“Nimefurahishwa na mafundi lakini sijafurahishwa na namna ujenzi ulivyo katika hatua za nyuma sana ukilinganisha na maeneo mengine hivyo basi naagiza katika kipindi hicho cha mwezi mmoja mkamilishe na ikibidi nitakuja kukifungua mwenyewe kituo hiki,”alisema Jafo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: