Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kuna hazina ya kutosha ya mafuta ghafi ya kula nchini.

Waziri Mwijage ametoa ufafanuzi huo Jana Mei 07, 2018 baada ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia kutaka kauli ya serikali kuhusu ukweli wa taarifa za kwenye vyombo habari kuhusiana na mafuta ya kula.

"Sasa hivi kwenye hifadhi ya mantenki ya mafuta ghafi ya kula Jiji Dar es Salaam kuna mafuta ya maweze takribani tani 40,000 na meli zilizopo nje zina CPO tani 50,000. Kiwango kilichopo kwenye hifadhi na yaliyopo kwenye meli kuna mafuta ghafi tani 90,000 ila kinacholetana tatizo ni kutokubaliana katika viwango vya kodi", amesema Mwijage.

Pamoja na hayo, Mwijage ameendelea kwa kusema "kwa mujibu wa sheria, muagizaji wa mafuta kutoka nje anatozwa kodi ya asilimia 10 lakini vipimo vinamuonesha Kamishna wa Forodha kwamba mafuta hayo ni ghafi na si yaliyosafishwa hivyo anayachukulia ni mafuta safi na kutoza kodi ya asilimia 25".

Awali Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba alilieleza Bunge kuwa serikali inalifanyia kazi suala la mafuta ya kula ili wananchi wasiyakose au yasipande bei sana na kwamba, serikali inaruhusu mafuta ghafi kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya walaji kwa kuwa kiwango kinachozalishwa nchini hakitoshi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: