Monday, 14 May 2018

Wananchi Watishia 'Kumuua' Mwalimu Mkuu, Wanamtuhumu Kuwachapa Wanafunzi na Kuwalimisha Shamba Lake


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wazazi wa kata tatu wilayani hapa Mkoa wa Mara, wamemtaka mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nyanungu, Otieno Nicholaus kuchagua kuhama au kupoteza maisha.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa mkutano wa wazazi uliofanyika hivi karibuni shuleni hapo.

Wazazi hao walimtuhumu mwalimu huyo kwa kuwapiga watoto hadi kuwajeruhi wanapokataa kulima shambani kwake.

Mmoja wa wazazi wa watoto wanaodaiwa kupigwa, Muniko Sibora alisema Mei 7 mwalimu huyo alimpiga mwanaye baada ya kuvaa yeboyebo kutokana na kuwa na kidonda mguuni.

Pia, alisema aliwapiga watoto wa Mwita Nyasongo na Ngocho Matiku kwa kuwa hawakwenda na majembe kupalilia mahindi yake.

“Huyu mwalimu anachofanya siyo sahihi, anatakiwa ahame vinginevyo mambo yatamharibikia,” alisema.

Kaimu ofisa elimu wilaya, Hawamu Tambwe alikiri kupata taarifa hizo na kwamba amemtuma mratibu elimu kata kufuatilia undani wa suala hilo na kupata taarifa ya maandishi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyanungu, Turuka Magabeu alikiri kupokea malalamiko ya wazazi kuhusu mwalimu huyo kuwapiga watoto. 

“Inaelezwa katika tukio la mwisho aliwapiga na kuwaumiza watoto watatu kiasi cha kupelekwa hospitali,” alisema Magabeu.

Naye mjumbe wa kamati ya shule hiyo, Museti Mwikwabe alisema Aprili 30 aliitisha kikao cha kamati lakini wajumbe walikataa wakiwamo wazazi wote.

“Mei 4 aliwapeleka shambani watoto wakati wa masomo na tukamweleza, akaja juu na Mei 7 akaamua kuwapiga na kuwaumiza watoto huku akiwaambia waje watueleze wazazi,” alisema.

Mwalimu Otieno hakuweza kupatikana shuleni hata simu yake ilikuwa haipatikani kwa kile kilichodaiwa kuwa anaishi kwa kujificha.

Akizungumza suala hilo, diwani wa Kyambahi, Mtoni Manyaki alikiri kupata taarifa hizo na ameitisha kikao cha kamati ya maendeleo kata Mei 21 ili kulijadili.

Naye mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya, Juma Hamsini alisema baada ya kupata taarifa ameagiza timu yake kuchukua hatua haraka na tayari wamepiga marufuku kuwatumia wanafunzi kulimia walimu.

“Hivi karibuni katika Shule ya Msingi Mlimani kulikuwa na kesi kama hiyo niliandika barua ya kupiga marufuku, wanafunzi wanaweza kulima shamba la shule tena si wakati wa masomo,”alisema.

Polisi wilayani hapa wanadai wanaendelea kumsaka mwalimu huyo kuhusiana na tuhuma zilizowasilishwa.

No comments:

Post a Comment