Wednesday, 23 May 2018

Tibaijuka: Kwa Hili Serikali ni Lazima Iwajibike.....Utawala wa Sheria Uheshimiwe

Mbunge wa Muleba Kusini(CCM), Profesa Anna Tibaijuka ameitaka serikali ya awamu ya tano iwajibike kuwanunulia ng'ombe wafugaji walioshinda kesi zao Mahakamani kama sheria inavyosema nasio vinginevyo.

Prof. Tibaijuka ametoa kauli hiyo jana  Mei 22, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 34 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasiri na Utalii ya mwaka 2018/19 ambayo ni shilingi 115.8 bilioni baada ya kuwepo tatizo la muda mrefu kwa wafugaji kuporwa mifugo yao na watu wa maliasili pindi wanapokuwa wamevamia hifadhi kwa lengo la kulisha mifugo yao.

"Serikali hii ya awamu ya tano naishukuru sana walitoa miezi 10 kwa Mawaziri humu ndani Bungeni kutafuta ardhi za wafugaji lakini hiyo kazi haikufanyika kilichotokea watu walikuja kuondolewa kwenye hifadhi kama operesheni na kwa kweli yalikuwa mateso makubwa sana. Mhe. Spika ni utawala wa sheria kama mtu ameshinda mahakamani na anatakiwa arudishiwe mifugo yake ni lazima afanyiwe hivyo na kama haipo lazima inunuliwe, serikali hapo inatakiwa kuwajibika", alisema Tibaijuka.

Pamoja na hayo, Prof. Tibaijuka aliendelea kwa kusema "kuwajibika hakuwezi kuwa sehemu ya wananchi pekee yake bali na serikali yenyewe lazima iwajibike pale ambapo kosa limefanywa na watendaji wake".

Kwa upande mwingine, Profesa Anna Tibaijuka amesema hawezi kuiunga hoja iliyokuwa mezani mpaka pale suala lake litakapopatiwa majibu yenye kuridhisha.

No comments:

Post a Comment