Serikali imesema tayari nchi imeanza rasmi majaribio ya dawa kinga mpya inayozuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi (PrEP), huku ikikanusha kuwapo kwa dawa inayotibu ugonjwa huo.

Dawa kinga hiyo mpya  ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ikiwa mtumiaji atameza kila siku kwa muda wa siku saba kabla hajashiriki tendo la kujamiiana, ataendelea kumeza kwa kipindi chote atakachokuwa katika hatari ya kuambukizwa.

Hayo yamesemwa leo Mei 9, 2018 mjini Dodoma na naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile wakati  wa uzinduzi wa mpango wa nne wa VVU na Ukimwi katika sekta ya afya (HSHSP IV 2017-2022) sambamba na maadhimisho  ya miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.

Amesema taarifa kwamba nchi inazindua tiba dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, si sahihi kwani Tanzania haijapata tiba hiyo.

"Kinachoendelea tumezindua dawa kinga, kuna dawa ambayo tunataka tuielekeze katika makundi ambayo tunayaona yapo kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi, watapatiwa kwa lengo la kuwakinga wasipate,” amesema Dk Ndugulile na kuongeza:

“ila sio suluhisho na tuseme vilevile kwamba hatujapata tiba ya virusi vya Ukimwi na utaratibu huu wa dawa kinga, ndiyo inaanza majaribio sasa  na haijaanza kupatikana.”

Dawa hizo mpya zenye uwezo wa kukinga maambukizi dhidi ya VVU kwa asilimia 99, zilizoanza kutumika katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika, zinakuja wakati ukanda huo ukiongoza duniani kwa kuwa na asilimia 50 ya waathirika wote duniani.

Utafiti uliofanywa na mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha London, Dk Sheena McCormack umeonyesha kuwa PrEP inazuia maambukizi ya Ukimwi kwa kuua virusi baada ya kufanyiwa majaribio na kundi la wapenzi wa jinsia moja, ambao wamo katika hatari zaidi ya maambukizi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetambua kwamba dawa hiyo ya tembe inaweza kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: