Bunge  limesema wabunge 363 hawatasafiri kwenda popote nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano kutokana na sera ya kupunguza safari za kimataifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Spika wa Bunge Job Ndugai bungeni alipokuwa akijibu mwongozo wa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari.

Katika kauli yake, Nassari aliomba mwongozo wa Spika kutokana na uwakilishi wa Bunge kuwa hafifu "kidogo" kwenye majukwaa ya kimataifa.

"Ushiriki wao majukwaa mbalimbali wabunge wamekuwa wakienda kwa gharama zao... wanajilipia ndege, kampeni kwa gharama zao, wakati mataifa mengine kama Cameroon na wapi wametuma ujumbe wa watu kabisa kwenda kutafuta nafasi, naomba muongozo wako kwenye hili," alisema Nassari.

Nassari alisema juzi Bunge limewapongeza Mbunge wa Handeni Vijijini (CCM), Mboni Mhita ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Vijana wa Bunge la Afrika na Mbunge wa Shinyanga mjini (CCM), Steven Masele ambaye amechaguliwa kuwa Makamu wa Kwanza na Rais wa Bunge la Afrika (PAP), lakini ushiriki wa bunge ni hafifu kwa wabunge wanaotakiwa kushiriki kwenye majukwaa ya kimataifa.

Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema sera ya kupunguza safari za nje, imepunguza safari za wabunge kwa zaidi ya asilimia 90.

"Zimeelezwa mara kwa mara sababu za safari kupungua ndio mtazamo wa nchi na uelekeo wa nchi, hata mkuu wa nchi yeye mwenyewe ni mfano wa kutosafiri nje," alijibu Spika Ndugai.

"Sasa kundi linalobakia la kusafiri nje ya nchi angalau ni IPU (Bunge la Muungano wa Mabunge) ambalo lina wabunge sita, SADC yenye wabunge watano, PAP (Bunge la Afrika) yenye wabunge wanne, ACP (Bunge la Afrika, Caribean na Pacific) ambayo ina wabunge watatu, CPA (Madola) yenye wabunge watano... Ukiwajumlisha wote hawa ni takriban 30 na bunge lina wabunge 393. Ukiondoa hawa 30 wanabaki wabunge 363 ambapo kwa miaka mitano hawatasafiri kwenda popote," alisisitiza.

Ndugai alisema wabunge hao labda watasafiri kwa safari ambazo hazina gharama yote kwa mlipa kodi.

"Labda vile visafari ambavyo huwa havina chochote ambavyo huwa tunawauliza kuna safari hapa unaweza kutembea kidogo," alisema Ndugai.

"Vile ambavyo havihusishi serikali, tumekuwa tukiokota mmoja mmoja... wengine wanakataa."

Alieleza kuwa kuna wakati ilipatikana safari ya kwenda China wabunge 20 lakini walipofika Uwanja wa Ndege, wabunge sita au saba hawakuwapo.

"Wanasema aaah, Spika bwana hizo safari zao za njaa njaa hatuendi sisi, sasa panapokuwa na wabunge 30 kati ya 393 halafu hawa 30 kila wakati wanatushughulisha kujibu kwanini wao hawasafiri hapo ndio naonaga ni 'very unfair' (si haki kabisa)... tunashughulika nao ofisini tunaelezana ikiwezekana wanaenda na kadhalika."

Spika alifafanua wabunge hao wasifanye kuwa wanastahili sana kusafiri.

"Inategemeana na mambo kadhaa, bajeti yetu na mambo mengine kwa hiyo bajeti yetu ikiruhusu wataenda inapokuwa imebana na mambo mengine kidogo haijakaa sawa kikao hiki mnakosa kikao kinachokuja mnaenda," alisema spika huyo.

"Hivyo hivyo tunavyoenda. Ukiwa katika kundi ambalo wenzako hawaendi popote, lakini wewe angalau unasafiri kidogo halafu nyie ndio wakuuliza maswali kila kukicha haipendezi."

Aliagiza mambo ya aina hiyo yamalizwe kiutawala na kwamba wataendelea kusafiri hao wachache kutegemeana na hali halisi na mambo yalivyo mezani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: