Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali mkoani Simiyu imesema imekusudia kuiimarisha shule ya Sekondari ya Bariadi ambayo ilitengwa kuwa Shule ya Michezo, kwa kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike na wa kiume na kuiwekea miundombinu yote muhimu,  ikiwemo viwanja vya michezo yote kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipokuwa akifunga mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kimkoa katika viwanja vya Shule ya sekondari ya Wasichana Maswa.

"Ningehitaji tuifanye Shule ya Sekondari Bariadi kuwa shule maalum ya kimichezo ya Kimkoa, yenye mabweni ya wavulana na wasichana na tuiwekee miundombinu yote ya michezo ili watoto wote wenye vipaji vya michezo waende pale na nitaomba kibali walimu wa michezo wahamie hapo,  tufike mahali ambapo Bariadi Sekondari itatoa wachezaji wa kutumainiwa kwenye Taifa" amesema Mtaka.

Aidha, amewataka wanafunzi wote kuwa na mtazamo tofauti katika michezo kwa kuondokana na nadharia ya kuwa michezo ni afya, burudani na kwenda kwenye dhana ya michezo kama taaluma, ajira na biashara, ambapo amehimiza kuwa mkoa huo utafanya uwekezaji na mapinduzi ya michezo kibiashara katika Shule hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewataka wanafunzi hao kuuwakilisha vema mkoa na kuwatakia heri na ushindi katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA ngazi ya Taifa yatakayofanyika jijini Mwanza, huku akiwataka kuwa na nidhamu kipindi chote watakachokuwa huko na akaahidi kutoa zawadi mbalimbali kwa washiriki wote watakaporudi na ushindi.

Katika hatua nyingine Mtaka akiwakabidhi walimu na wanafunzi jezi na trakisuti  zilizotolewa zenye zaidi ya shilingi milioni mbili kwa udhamini wa Kiwanda cha Chaki (MASWA CHALKS), amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi mkoani humo kujipanga kwa ajili ya kudhamini mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA mwaka 2019 kupitia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kuendelea kuutangaza mkoa huo.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory amesema changamoto kubwa zilizowakabili washiriki wa mashindano hayo ni pamoja na upungufu wa viwanja katika shule za msingi na sekondari na kukosa wafadhili kutoka nje ili kuwezesha wanafunzi kukaa kambini muda mrefu kujiandaa na mashindano.

Kwa upande wao wanafunzi/ washiriki wa UMISSETA na UMITASHUMTA mkoa wa Simiyu wamemhakikishia Mkuu mkoa na wananchi kwa ujumla kuwa watarudi na ushindi katika mashindano hayo Kitaifa.

"Mwaka 2018 tumejipanga na ushindi ni lazima kwa mwaka huu sisi tunaenda Mwanza kushinda na kuchukua makombe, tunamhakikishia Mkuu wa Mkoa  na wananchi wote wa Simiyu kuwa tunarudi na ushindi" Alisema Mwanaidi Khamis kutoka  Maswa.

Jumla ya washiriki 811 wa michezo mbalimbali kutoka katika Halmashauri zote Sita za Mkoa wa Simiyu wameshiriki mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa kwa mwaka 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: