Serikali imesema itawalipa mawakala wote wa pembejeo za kilimo baada ya vyombo vya uchunguzi kukamilisha uchunguzi wa watumishi waliodanyanga kuhusu malipo na uhakiki wa madeni unaendelea.

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliozitoa wakati wakijadili bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2018/19, jana jioni Mei 16, 2018, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema malipo ni mara baada ya uchunguzi kukamika.

“Nani kaiibia Serikali, katika maombi haya vyombo vya uchunguzi vipo kazini, sisi kama wabunge wasimamizi wa rasilimali, vyombo vya uchunguzi ni muhimu na kama ni mtumishi nani aliongeza sifuri katika milioni 20 ikawa bilioni, fedha si tatizo na tutawalipa wote wanaoidai Serikali,” alisema Dk Kijaji

Kuhusu kutengwa kwa bajeti kidogo, Dk Kijaji alisema Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo lakini utengaji wa bajeti unategemea rasilimali zilizopo.

“Rasilimali ziko chache kuliko mahitaji, sote tupo hapa, mlisema bajeti ya afya iongezwe, maji iongezwe na ifahamike Serikali inatoa kipaumbele kwa kilimo na sisi tunatambua kuwekeza katika kilimo,” alisema Dk Kijaji

Alisema miongoni mwa jitihada hizo ni kuiwezesha Benki ya Kilimo: “Tumewekeza Sh60 bilioni na mpaka sasa wana Sh66 bilioni, wameweza kuongeza kiwango hiki katika utendaji wetu na tumechukua mkopo zaidi ya Sh250 bilioni na kuipa benki hii.”

Akigusia benki hiyo kuwa jijini Dar es Salaam, alisema mwezi huu itafungua tawi jijini Dodoma, Juni jijini Mbeya na Julai jijini Mwanza na dhamira yetu ni kuwafikia wananchi kule waliko.

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Joseph Kakunda alitoa maagizo kwa maofisa kilimo kutoka ofisini na kwenda kuelimisha wakulima na wale watakaoshindwa watachukuliwa hatua.

“Lazima wakulima wapate haki yao ya elimu kuhusu kilimo na utaratibu wa kusubiri posho ili aende kufanya kazi yake tumeshapiga marufuku,” alisema Kakunda.

Kakunda alisema, “maofisa ushirika lazima wahakikishe wanafanya mapitio ya vyama vya ushirika ili kujua kama utendaji ni mzuri na kama ni mbovu wavifute na kuvisajili upya.”

“Maofisa ugani wafanye kazi ya kuwatambua wakulima wote ili Serikali ifanye maandalizi ya haraka ya kuandaa pembejeo, walio chini ya Tamisemi wapate huko hizi taarifa na uzembe hautavumiliwa,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh29 bilioni kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na, “sisi kama wizara tutalisimamia hili na tunaahidi kushirikiana vizuri na wadau wa wizara ya kilimo.”
Share To:

Anonymous

Post A Comment: