Serikali imesema itaajiri watumishi wapya 207 kwa ajili ya Wizara ya Nishati katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai mosi.

Vilevile, imesema itawapandisha madaraja watumishi 100 wa wizara hiyo ambayo wamepata sifa za kitaaluma na wenye utendaji mzuri wa kazi.

Hayo yalielezwa jana bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, alipowasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema watumishi hao 207 wataajiriwa katika kada mbalimbali za wizara hiyo.

Alisema kati yao, 43 wataajiriwa wizarani, 116 katika Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na 48 kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura).

Aidha, Dk. Kalemani alisema ili kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu wazawa wa kutosha katika sekta ya nishati, wizara yake imeendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo kutoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania wanaokidhi vigezo kwenda kusoma nchi mbalimbali kwa ngazi ya shahada, uzamili na uzamivu.

Alisema kuwa kwa mwaka huu wa fedha, Watanzania 22 walipata ufadhili wa masomo kutoka Serikali ya China katika masuala ya mafuta na gesi asilia.

Vilevile, Waziri Kalemani alisema kupitia Programu za Uendelezaji wa Rasilimaliwatu katika sekta za mafuta na gesi, watumishi 16 walipata ufadhili katika fani mbalimbali zikiwamo za usimamizi katika masuala ya mafuta na gesi asilia, sheria pamoja na uhasibu na fedha.

"Kwa mwaka 2018/19, Watanzania 22 watapata ufadhili wa masomo kutoka Serikali ya Watu wa China," alisema.

Wakati huo huo, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, amesema wizara yake inaendelea kutekeleza agizo la serikali kuhamishia shughuli zake Makao Makuu Dodoma.

Alisema hadi sasa watumishi 50 kati ya 153 wa wizara hiyo wamehamia kwenye jiji hilo jipya.

Alisema wizara inaendelea kukamilisha taratibu husika ili watumishi wote wahamie Dodoma katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: