Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amesema uamuzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kumsimamisha masomo mwanafunzi wake wa mwaka wa tatu, Abdul Nondo unakitia aibu chuo hicho na ni kinyume na haki za binadamu.

Akizungumza jana Jumatatu Aprili 30, 2018 wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2018/19, Bobali alisema sheria iliyotumika kumsimamisha masomo inatakiwa kufutwa.

“Hivi ni wanafunzi wangapi ambao wameshtakiwa na kesi zao zipo mahakamani lakini wanaendelea na masomo. Hili suala la Nondo linakitia aibu chuo pengine watueleze tu kwamba jambo hili ni la kisiasa,” alisema Bobali.

Wakati Bobali akitoa maelezo hayo, mbunge wa Magogoni (CUF), Dk Ally Yusuf Suleiman aliomba taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na kubainisha kuwa hata wabunge wapo walioshtakiwa, wengine kufungwa lakini mpaka sasa bado wanaendelea na ubunge wao.

“Napenda kumpa taarifa mzungumzaji (Bobali) kuwa hata wabunge wapo walioshtakiwa lakini mpaka kufungwa lakini bado ni wabunge hadi sasa,”alisema Suleiman.

Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) amesimamishwa masomo kuanzia Machi 26, 2018 kwa barua iliyoandikwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye, aliyeeleza kuwa amesimamishwa kwa mujibu wa taratibu za chuo hicho.

Nondo alijikuta kwenye misukosuko na vyombo vya dola tangu alipotoweka katika kile kilichoelezwa kuwa ni katika mazingira ya kutatanisha Machi 6 na kuonekana Machi 7 wilayani Mufindi, Iringa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: