Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF, Wallace Karia amezitakia kila la heri timu zote 28 zinazoanza kibarua cha kutafuta nafasi ya kupanda daraja kutoka katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa(RCL) inayotarajia kuanza Mei 6 na kumalizika Mei 22,2018 kwenye vituo vinne.
Rais wa TFF Ndugu Karia amezitaka timu zote kupambana uwanjani na wachezaji kuzingatia nidhamu ili kuongeza ushindani wa mashindano hayo na kupata matokeo mazuri yatakayoziwezesha kufikia lengo la kupanda daraja,huku akisisitiza timu zote kufuata sheria na kanuni za mashindano.
Rais wa TFF Ndugu Karia amewataka waamuzi watakaochezesha mashindano hayo katika vituo vyote vinne kuzingatia haki na sheria za Mpira wa miguu bila hiyari ili kuwapata washindi sahihi wanaostahili na pia Waamuzi wenyewe kujiweka katika nafasi ya kuangaliwa maendeleo yao na uwezekano wa kupandishwa katika madaraja ya juu.
Aidha amewataka viongozi wote wanaohusika na wasimamizi kusimamia haki na kuhakikisha sheria na kanuni zinafuatwa pasipo upendeleo na dhuluma kwa yeyote.
 “Nasisitiza kwa timu zote,viongozi,wasimamizi na waamuzi kufuata sheria,kanuni na taratibu za mashindano tunahitaji kuona ushindani kutoka kwao ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni na taratibu za mashindano lakini waamuzi nao wachezeshe kwa haki kwa kufuata sheria za mpira wa miguu,TFF tutakuwa wakali kwa yeyote atakayekwenda kinyume na sheria,kanuni na taratibu za mashindano”.amesema Rais wa TFF Ndugu Karia.
Ligi ya RCL itakayoshirikisha timu 28 itachezwa katika vituo vinne vya Geita,Rukwa,Singida na Kilimanjaro kila kituo kikiwa na kundi moja lenye timu 7.
Timu 2 za juu kutoka kila kundi zitapanda daraja kwenda kucheza Ligi Daraja la Pili msimu unaofuata wakati timu zitakazosalia katika kila kundi zitarejea kucheza Ligi katika mikoa yao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: