Mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Leodegar Tenga amesema baadhi ya wenye viwanda wana hofu ya kushiriki shindano la mzalishaji bora wa mwaka wakidhani wataharibu masoko yao iwapo hawatashinda.

Hata hivyo, Tenga aliwatoa hofu kwamba tuzo hizo hazina uhusiano wa moja kwa moja na ubora wa bidhaa, bali wanaangalia vigezo vingine muhimu katika uzalishaji na namna wenye viwanda wanavyoweza kujifunza kutoka kwa wenzao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Tenga alisema katika tuzo za Rais za mzalishaji bora wa mwaka 2017 zinazotarajiwa kufanyika Mei 4, ni wenye viwanda 36 waliojitokeza kushiriki shindano hilo.

Tenga alibainisha kuwa mwitikio umeongezeka kidogo ikilinganishwa na mwaka jana, lakini akasisitiza kwamba kampuni kubwa hazitaki kushiriki kwa kuhofia kuharibu taswira iwapo hazitashinda.

“Changamoto kubwa ni hawa wazalishaji wakubwa, ukiwafuata wanakwambia hawatashiriki wakihofia kuharibu taswira za kampuni zao,” alisema Tenga na kuongeza:

“Tunajitahidi kuwaeleza kuwa mashindano hayo ni muhimu kwao na hayahusiani na ubora wa bidhaa zao hivyo wanatakiwa kushiriki kuonyesha ukuaji wa uzalishaji wao.”

Awali, mwenyekiti wa CTI, Dk Samwel Nyantare alisema kwamba tuzo hizo zitatolewa kwa sekta 17 zinazotambulika kimataifa na mwaka huu wameongeza sekta moja ya matumizi bora ya nishati.

Alizitaja baadhi ya sekta zitakazoshindaniwa kuwa ni vinywaji, ujenzi, kemikali, nishati, plastiki, fedha, mbao na samani, chuma, magari, usafirishaji, karatasi, dawa na vifaatiba, nguo na bidhaa za madini.

Naye mkurugenzi wa machapisho na mawasiliano wa CTI, Thomas Kimbunga alibainisha kuwa vigezo vilivyotumika kuwapata washindi wa kila sekta ni pamoja na utendaji wa kiuchumi, utendaji wa kiteknolojia, matumizi ya nishati, uuzaji bidhaa nje ya nchi, usalama sehemu ya kazi na kuzingatia masuala ya kijamii.

Kuhusu mshindi wa jumla, Kimbunga alisema kwamba wataangalia vigezo vingine kama mizania ya jinsia kwenye ngazi ya utawala, uhifadhi wa mazingira, uhusiano mzuri, kuzingatia viwango vya ubora na uhusiano na sekta nyingine za uchumi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: