Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempigia simu Katibu Mkuu wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo mbele ya wananchi wa kijiji cha kidodi , kumtaka kumchukulia hatua mkandarasi aliyepewa mradi wa maji na kutoukamilisha.

Akizungumza kwa sauti kubwa huku wananchi wa Kidodi wakiwa wanasikiliza 'live', Rais Magufuli amesema kwamba mkandarasi huyo alishapewa pesa za mradi milioni 800 lakini maji hayajafika kwa wananchi, hivyo ahakikishe amechukuliwa hatua za kisheria au awepo eneo la mradi kukamilisha.

Awali kabla ya kupiga simu hiyo, Rais Magufuli ametuma salamu kwa mkandarasi huyo kupitia wananchi wa kijiji cha Kidodi, kumtaka azirejeshe fedha alizopewa za mradi pasipo kutekeleza mradi huo muhimu kwa jamii.

“Nafahamu kuna mradi wa maji wa milioni 800 na mkandarasi alipewa, lakini maji hayajafika kwa wananchi, nilidhani mbunge wenu atauliza achukuliwe hatua gani lakini hajauliza, na mkandarasi kama alikula hela atazitapika, naomba mumfikishie huu ujumbe”, amesema Rais Magufuli.

Baada ya simu hiyo Profesa Mkumbo amesema anatarajia kuanza safari mchana huu kwenda kijijini hapo kushughulikia tatizo hilo, na mpaka kesho atakuwa ameshafika eneo la tukio na kutoa suluhu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: