Makhtar Diop, raia wa Senegal ameteuliwa kuwa makamu wa rais wa Benki ya Dunia (WB) atakayekuwa anasimamia miundombinu.

Diop alitangazwa kushika nafasi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo kumfanya kuwa miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu wa taasisi hiyo muhimu duniani.

Taarifa iliyotolewa na benki hiyo inasema Diop anayaanza majukumu hayo mapya baada ya kuwa Makamu wa Rais anayesimamia Afrika katika miaka sita iliyopita akifanikisha kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya Dola 70 bilioni za Marekani.

Ndani ya miaka hiyo sita, Diop alisimamia miundombinu ya usafiri na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), nishati na madini, fedha na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP).

‘Katika majukumu yake mapya, Diop atasimamia ufadhili wa miundombinu ya fedha katika ufanikishaji wa maendeleo endelevu hivyo kupunguza tofauti iliyopo kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Uteuzi wa Diop anayetajwa kuwa miongoni mwa Waafrika 100 wenye ushawishi zaidi duniani utaanza Julai Mosi.

Alipokuwa akiisimamia Afrika, inaelezwa alisimamia upatikanaji wa fedha za kufanikisha miradi ya aina tofauti akihamasisha zaidi ubunifu na uvumbuzi wa kisayansi.

Alihakikisha Afrika inapata umeme wa uhakika na nafuu huku ikiunganishwa kwa barabara zinazopitika wakati wote.

Ndani ya benki hiyo, Diop ameshahudumu kama mkurugenzi wa fedha, sekta binafsi na miundombinu Amerika Kusini na Visiwa vya Caribbean.

Kati ya mwaka 2009 na 2012 alikuwa mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Brazil ambako alisimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Alishawahi kuwa Mkurugenzi Mkazi katika nchi za Kenya, Eritrea na Somalia.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: