Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa anayeshughulikia Elimu Tixon Nzunda akizungumza katika kikao cha baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Tamisemi. 

 Washiriki wakimsikiliza kwa makini Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda.
 Washiriki wakimsikiliza kwa makini Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda.
Washiriki wakimsikiliza kwa makini Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda.

.......................................................................
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda amewaasa watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea ya kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika jana katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, nje kidogo ya jiji la Dodoma, Bwana Nzunda alisema kuwa kutokana na Ofisi hiyo kupewa majukumu makubwa ya kiutendaji, watumishi wana wajibu wa kufanya kazi kwa kushirikiana katika kujenga umoja wa ofisi hiyo.

Alisema kuwa watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI wanapaswa kuzingatia maadili na misingi ya utoaji huduma bora na kujiepusha na vitendo vya rushwa na wakumbuke kuwa Ofisi hiyo ipo chini ya Mheshimiwa Rais, na hivyo wanajukumu la kumwakilisha Rais vizuri katika utoaji wao huduma kwa wananchi.

Pia aliwashauri watumishi hao kujiepusha na vitendo vitakavyopelekea kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na magonjwa mengine sugu na pia aliwahimiza kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuwa na afya njema itakayowawezesha kufanya kazi zao vizuri.

Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu amewapongeza wafanyakazi bora wa Ofisi ya Rais TAMISEMI waliochaguliwa kwa mwaka 2018, ambapo pia aliagiza wafanyakazi hao wapewe zawadi zao bila kucheleweshwa ifikapo kesho.

Pia alimpongeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe kwa maelekezo yake yaliyofanikisha kazi kubwa ya kuandaa bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI mwaka 2018.

Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali watu bwana Mrisho Mrisho alimweleza Naibu Katibu Mkuu na wajumbe wa baraza la wafanyakazi kuwa kutokana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuongezewa majukumu ya utendaji kazi, idadi ya watumishi katika ofisi hiyo imeongezeka na kufikia watumishi 678 hivi sasa.

Alisema kuwa idadi hiyo imejumuisha watumishi kutoka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na watumishi wengine wanaokuja kuimarisha idara mbalimbali za TAMISEMI.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE)  Mkoa wa Dodoma bwana John Mchenya aliwataka viongozi wa tawi la Tughe kutoka Ofisi hiyo kufanya vikao vya mara kwa mara na watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI  ili wahamasike kujiunga na chama hicho.

Bwana Mchenya alisema kuwa yeye binafsi atakuwa mstari wa mbele kushiriki katika vikao hivyo ili waweze kuwahamasisha watumishi wengi wanaofanya kazi TAMISEMI ambao wametoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kujiunga na chama hicho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: