Nyota wa kimataifa wa Tanzania na mchezaji wa zamani wa Yanga, Simon Msuva amekutana kwenye jiji moja na klabu yake hiyo ya zamani ambayo ipo kwenye majukumu ya mechi za kimataifa kama ilivyo kwa klabu yake ya sasa Difaa El- Jadidi.

Msuva yupo jijini Algiers na klabu yake, Difaa  El- Jadidi kwa ajili ya mchezo wao wa ufunguzi hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Mouloudia Club D'Alger Saa 4:00 usiku wa leo.

Wakati Yanga nao wamewasili mjini humo leo kwa ajili ya mchezo wao wa ufunguzi wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya U.S.M. Alger utakaofanyika Jumapili Mei 6.

Msuva akiwa kwenye msimu wake wa kwanza ndani ya Difaa Hassan El- Jadidi amekuwa na msimu mzuri kwenye ligi ya Mabingwa Africa ambapo hadi sasa amefunga mabao 5 kwenye michuano hiyo. Difaa  El- Jadidi ipo Kundi B na D'Alger, E. S. Setifienne ya Algeria na TP Mazembe ya DRC.

Yanga na U.S.M. Alger zipo Kundi D la Kombe la Shirikisho pamoja na Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya ambazo zitamenyana zenyewe katika ufunguzi wa hatua ya 16 Bora ya Kombe Shirikisho Afrika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: