MKE anadaiwa kumuua mumewe, Ahmed Salim kwa kumchoma kisu baada ya kumlazimisha kurudi jikoni kupika chakula baada ya kutoshiba mkoani Mtwara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya, alisema tukio hilo lilitokea juzi mkoani humo ambapo mwanamume huyo alikufa papo hapo baada ya kuchomwa kisu na mke wake.

Alisema siku ya tukio majira ya saa 1:30 usiku, mwanamke huyo alimuandalia mume wake chakula na kumpatia.

“Kile chakula kilikuwa kidogo, mume wake, Ahmed Salim, alimtaka arudi jikoni kwa ajili ya kupika tena chakula kwa kuwa hakikumtosha. Hapo ndipo palitokea ugomvi wakalumbana na wakaendelea kugombana, mke alichukua kisu na kumchoma kifuani na kufariki dunia papo hapo baada ya kutokwa na damu nyingi kwenye jeraha.” alisema Kamanda Mkondya.

Aidha, alisema katika tukio hilo wanamshikilia na kijana mmoja ambaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini kutokana na uchunguzi unaoendelea kwa alikuwepo katika tukio hilo, hivyo watakapopata maelezo yatakayojiridhisha kutohusika ataachiwa.

“Bado huyu kijana tunamhoji ni kwa nini hakutoa msaada wa kuamua ugomvi huo. Hapa tunataka kujua na yeye amehusika au la na kwa huyu mwanamke taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema.
Aidha, Kamanda alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala kwa ajili ya kusubiri taratibu za mazishi
Share To:

msumbanews

Post A Comment: