Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu amesherehekea siku yake ya kuzaliwa akiwa gerezani huku familia yake ikiisherehekea kwa kula chakula pamoja na watoto yatima wanaolelewa katika Kituo cha Nuru, Uyole jijini Mbeya.

Sugu ambaye anafikisha umri wa miaka 46, alisherehekea siku hiyo akiwa gerezani ambako anatumikia kifungo cha miezi mitano.

Keki ya mbunge huyo ilipambwa kwa kuchorwa pingu, mnyororo na taswira ya chumba cha Magereza.

Sugu alihukumiwa kifungo cha miezi mitano baada ya kukutwa na hatia ya kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, Februari 26.

Mwingine aliyehukumiwa kifungo hicho ni Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga ambao wote wanatumikia kifungo cha miezi mitano jela katika Gereza Kuu la Ruanda jijini hapa.

Jana, uongozi wa Hoteli ya Desderia inayomikiliwa na Sugu ulisherehekea siku hiyo pamoja na watoto yatima wa Kituo cha Nuru na kula nao chakula cha pamoja.

Hilo ni agizo la Sugu kuendelea kuwa karibu na jamii ya wakazi wa Mbeya.

Mke wa Sugu, Happiness Msonga alisema mumewe ndiye aliyeagiza siku ya kuzaliwa kwake iadhimishwe pamoja na watoto yatima kwa kula nao chakula.

“Sugu amesema anawapenda sana watoto na yupo pamoja nao licha ya kuwa yupo gerezani, lakini kiroho yupo nao daima. Ameagiza jana kwa kuwa pia ni Mei mosi, ni vyema tukashiriki sherehe hiyo na watoto yatima,” alisema.

Happiness alisema Sugu kupitia uongozi wa hoteli yake wameanzisha mpango maalumu wa kutembelea na kujumuika na vituo vya watoto yatima vilivyopo jijini Mbeya kila mwisho wa mwezi kwa kuwapelekea chakula na misaada mingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Yatima cha Nuru-Uyole, Jarson Fihavango alimshukuru mbunge huyo na uongozi mzima wa hoteli yake kwa kuwapelekea chakula na misaada mingine watoto wanaowalea kituoni hapo.

“Tunajua mbunge wetu alipatwa na matatizo, lakini pamoja na kwamba yupo gerezani, lakini bado anawakumbuka wananchi wake. Sisi tunashukuru sana kwa hiki alichotufanyia,” alisema Fihavango.

“Tunasema aendelee na moyo huohuo na sisi tunamuombea. Hiki alichokifanya kina baraka kubwa mbele za Mwenyezi Mungu, tunajua namna anavyoweza kumlipa.”
Share To:

msumbanews

Post A Comment: