Friday, 18 May 2018

MBUNGE AMBARIKI MO DEWJI KUICHUKUA SIMBA


Mbunge wa Sengerema na Mwenyekiti wa Bunge Sports, William Ngeleja.

WAKATI zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya Simba kukutana kwa ajili ya mkutano wake wa mwisho juu ya kubadili uendeshaji wa klabu hiyo, Mbunge wa Sengerema na Mwenyekiti wa Bunge Sports, William Ngeleja amesema kuwa anakubaliana na suala la mabadiliko hayo.

Ikiwa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu yatafanikiwa yatamuwezesha mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ kuwekeza ndani ya timu hiyo.
Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.

Simba wapo kwenye mchakato huo wa mabadiliko wa uendeshaji wa klabu ambapo watatoka kwenye mfumo wa miaka mingi wa uanachama na kuingia kwenye mfumo wa hisa, huku Mo Dewji ndiye mfanyabiashara ambaye anataka kuwekeza ndani ya kikosi hicho.

Mfumo huo ukipita Mo Dewji ataruhusiwa kuchukua asilimia 49 ya hisa huku wanachama kwa umoja wao wakigawana asilimia 51.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ngeleja ambaye ni shabiki wa Simba amesema kuwa kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo ili kuleta maendeleo na inapaswa kuigwa na timu nyingine kwa maendeleo zaidi wakiwemo wapinzani wao, Yanga.

“Nafahamu mchakato huu una mkono wa serikali, mimi nawatakia mafanikio tukaamue jambo liende na tukamilishe zoezi hili baada ya muda mrefu, turuhusu sekta binafsi ziingie lakini kwa kiwango ambacho serikali wameona kwa sababu kulikuwa na mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

“Ni hatua nzuri ambayo inachukuliwa kwa sababu kuna maendeleo ndani yake kama likipita na nadhani klabu nyingine zinatakiwa zibadilike ikiwemo watani zetu Yanga, ili tusonge mbele ni lazima tukubali mchakato huu upite kama ambavyo klabu kubwa duniani ambavyo wamekuwa wakifanya,” alisema.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Ilala, Iddy Zungu alisema: “Ni furaha kubwa kuwa mabingwa na malengo ya timu inabidi yawe ya kuweka ushindani kwenye mashindano ya kimataifa ambako huko wanawakilisha taifa hivyo kuna haja ya Watanzania kuipa sapoti timu ya Simba ili iweze kusonga mbele na kupata matokeo mazuri.”

No comments:

Post a comment