Thursday, 10 May 2018

Mbowe Atua Mbeya Kuongoza mapokezi ya Sugu anayetoka jela

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda na viongozi wengine wa chama hicho wamefika Gereza Kuu la Ruanda mkoani Mbeya kuwapokea Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga.

Viongozi hao wamefika gerezani leo Mei 10, 2018 saa 12:45 asubuhi na kuingia ndani ya uzio wa gereza ambako askari wamewaondoa. Mbowe na wenzake wametii amri hiyo.

Wengine waliofika gerezani ni Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani.

Askari wamefika gereza kuu kuimarisha ulinzi wakiwa na magari mawili, moja limeingia ndani na lingine lipo nje.

Sugu na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Wawili hao wameshatumikia adhabu hiyo kwa siku 73 ikiwa ni zaidi ya robo ya kifungo chao.

No comments:

Post a Comment