Monday, 7 May 2018

Jaji Mkuu: “Tunataka hukumu kuanza kutolewa kimtandao”

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma amesema kutokana na ukuaji wa teknolojia hukumu haziwezi kupatikana kwenye makaratasi bali mitandaoni ili Jaji akikosea kitu dunia nzima ijue.

Jaji Prof Ibrahim ameyasema hayo wakati akizindua mafunzo endelevu kwa Majaji wapya 14 walioteuliwa hivi karibuni.

Amesema kuwa kazi ya Ujaji ni kazi ya kipekee kwani kesi zinakuwa ni tofauti hivyo lazima wapate mafunzo.

“Zamani kulikuwa na imani kwamba majaji lazima wajue sheria na hawahitaji mafunzo, lakini ukiangalia dunia ya sasa kuna mambo mengi duniani ikiwemo makosa mapya ya kwenye mitandaoni hivyo elimu endelevu kwa majaji ni lazima,” amesema.

Amesema kuwa ili Jaji aelewe sheria unayoitekeleza lazima ajue chimbuko la sheria anayotekeleza, hivyo lazima kuingia kwenye mfumo wa dijitali.

“Jamii inayotuzunguka imebadilika haiwezekani hukumu zikawa kwenye makaratasi tu bali ni lazima zitolewe na zipatikane haraka kwenye mitandao tena nimewaonya kwamba wakifanya kosa dogo tu dunia nzima itajua,” amesema Prof Jaji Ibrahim.

No comments:

Post a Comment