Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano katika klabu ya Simba, Haji Manara, ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitisha kikao maalum kwa ajili ya kujadili suala la Yanga kupoteza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilikuwa ina kibarua cha mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho katika hatua ya makundi dhidi ya USM Alger uliopigwa Jumapili iliyopita mjini Algiers, Algeria na wanyeji kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Manara ameliomba Bunge kuitisha kikao maalum kujadili namna Yanga ilivyofanya vibaya akieleza kuwa inawezekana suluhisho la tatizo hilo linaweza kupatikana.

Mbali na kuomba kikao kuitishwa bungeni kuijadili Yanga, Manara amesema amepokea matokeo hayo kwa masikitiko makubwa kutokana na kipigo ambacho watani zake wa jadi wamekipata huko Algeria.

"Ni matokeo mabaya, kusema tu ule ukweli yamenisikitisha hivyo ni vema wakajipanga kwa ajili ya michezo mingine inayofuata" alisema.

Kikosi cha Yanga kipo njiani hivi sasa kurejea nchini ambapo kinatarajiwa kuwasili majira ya kuanzia saa 6 mchana wa leo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: