Wednesday, 23 May 2018

Bajeti Maliasili na Utalii yapita, mradi wa Stigle’s Gorge watikisa

Sakata la mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge ambao utekelezaji wake unafanyika katika pori la akiba la Hifadhi ya Selous, liliibuka tena bungeni jana jioni Mei 22, 2018 na kuzua mvutano  huku Spika Job Ndugai akieleza kutoridhishwa na majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

Suala hilo lilitikisa Bunge jana mchana baada ya wabunge kadhaa kuhoji utekelezaji wa mradi huo, kueleza athari za kimazingira zinazoweka kujitokeza.

Selous ni miongoni mwa mapori yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (Unesco) kama sehemu ya urithi wa dunia, lakini uamuzi wa Serikali kuzalisha zaidi ya megawati 2,100 ikitumia zaidi ya Dola 2bilioni (zaidi ya Sh4.5trilioni) unaelezwa kuwa huenda ukaliondoa pori hilo kwenye orodha hiyo.

Bunge lilipokaa kama kamati jana jioni kupitisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2018/19 ya Sh115bilioni, mbunge wa Ulanga (CCM), Godluck Mlinga alianza kwa kuhoji kama Serikali itakuwa na mkakati mzuri wa kuwasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Hoja ya Mlinga iliungwa mkono na Ndugai aliyeitaka Wizara ya Nishati kuwa makini na kutengeneza utaratibu wa kupanda miti katika maeneo mbalimbali yanayoanzishwa miradi ya umeme.

Ndugai amesema katika maeneo mengi Wizara hiyo imekuwa na utaratibu wa kukata miti mingi katika utekelezaji wa miradi lakini inakosa usimamizi wa upandaji miti mingine.

“Mheshimiwa Mlinga  naamini kuwa wamekuelewa lakini na ninyi Nishati lazima muwe na mipango mizuri ya kupanda miti katika miradi yenu. Haiwezekani unakata miti lukuki lakini hakuna mpango wa kuipanda hiyo haikubariki kabisa,” amesema Ndugai.

Ndugai ambaye pia aliungwa mkono na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kwa pamoja walipingana na majibu ya Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kuhusu upandaji wa miti katika eneo hilo.

Wakati wawili hao wakitaka kusikia majibu ya Serikali kuhusu utunzaji wa mazingira katika eneo hilo, ikiwa ni sambamba na kupanda miti baada ya kuikata iliyopo, Dk Kalemani hakuwa akitoa majibu ya kina kuhusu hoja yao hiyo.

Katika majibu yake Dk Kalemani alisema miradi inayoanzishwa itakuwa na mipango mizuri hata ya uhifadhi wa mazingira, huku akijikita zaidi kueleza mpango wa kuongeza nguvu ya uzalishaji umeme nchini.

“Yaani Waziri hujatuelewa kabisa tunachotaka sisi ni hii  miti mingi mnayokata halafu mnakusanya na hampandi mingine, hivi hamjui habari ya uhifadhi kweli basi nimemaliza, nimemaliza waziri usisimame tena,” alisema Ndugai baada ya waziri huyo kuomba kujibu tena huku wabunge wakipinga.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola alisema mradi huo hauna madhara kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, akijitokeza mtu akaupinga atafungwa  bila huruma.

No comments:

Post a Comment