Wednesday, 16 May 2018

Atiwa Mbaroni Kwa Tuhuma Za Kukutwa Na Dawa Za Binadamu Zilizoisha Muda Wake

Jeshi la Polisi Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya linamshikilia mkazi wa Tabata Segerea Chama jijini Dar es Salaam Joseph Jaumbe( 52) kwa tuhuma za  kukutwa na dawa za binadamu kinyume na sheria huku zingine zikiwa zimepita  muda wake wa matumizi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP), Alhaj Kabaleke Hassan amesema kupatikana kwa mtuhumiwa huyo kumetokana na taarifa kutoka kwa wananchi kuwa anahifadhi dawa za kulevya ndipo wakafanya uchunguzi na nyumbani kwake hakuwa na dawa za kulevya kama walivyopata taarifa.

Amesema baada ya uchunguzi ndipo wakakuta ana dawa za binadamu zikiwa katika mifuko mbambali huku zingine zikiwa katika mfuko wa sandarusi.

Kamanda Hassan amesema kuwa baada ya kuwasiliana na Mamlaka Chakula na Dawa (TFDA) walipata dawa makopo 12 yenye vidonge 1000 ambazo hazijasajiliwa na mamlaka hiyo, dawa za Serikali makopo mawili ya vidonge 1000 , dawa  zilizoisha matumizi yake uzito wa kilo 25, dawa bandia zilizoisha muda wake makopo saba yenye vidoge 1000 , dawa za mashirika ya msaada makopo 12 yenye dawa 1000 kila kopo pamoja na vingashio za dawa mbalimbali.

Meneja wa Kanda ya Mashariki ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Emmanuel Alphonce amesema Jeshi la Polisi liendelee kufanya uchunguzi kwa mtu huyo kujua dawa anakozipata ili kubaini mtandao huo.

Alphonce amesema dawa hizo zingeingia mtaani zingeleta madhara kwa binadamu huku akishangaa kwa dawa hizo kufungwa mfuko wa kiroba pamoja na mifuko ya rambo. 
Amesema kuwa TFDA itaendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kulinda watanzania katika matumizi ya dawa , vifaa tiba na vitendanishi.

No comments:

Post a comment