Wednesday, 18 April 2018

Waziri Profesa Makame Mbarawa Afanya Ziara Ya Kushtukiza Shirika La Posta Tanzania Kukagua Utendaji

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Profesa Makame Mbarawa (MB)  jana  tarehe 17 Aprili, 2018 amefanya ziara ya kushtukiza Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania.

Mhe. Profesa Mbarawa ametembelea  Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania kwa lengo la kukagua utendaji na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Posta, katika ziara hiyo Mhe. Waziri aliongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Posta Luteni Kanali mstaafu Dr. Haruni Kondo.

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri alitaka kujionea matumizi ya mifumo ya kielektronik na namna ambavyo Shirika limejipanga kuitumia mifumo mbalimbali ili kusimamia utendaji kwa ukaribu.

Mhe. Waziri Mbarawa alitembelea idara ya Fedha, Idara ya Barua na Logistiki, Idara ya Sheria, Idara ya Masoko na pia alikagua mifumo  udhibiti wa gharama za mafuta na mwenendo wa magari ya Shirika yanayosafiri kati ya  Dar es salaam na mikoani.

Katika ziara hiyo Mh. Waziri ameitaka menejimenti ya Shirika kusimamia utendaji kazi na kuzingatia weledi na matumizi ya mifumo ya kielektroniki na kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia kasi ya Serikali ya awamu ya tano na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Mhe. Waziri alitoa msisitizo wa kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza ufanisi na kukuza tija kwa kila Idara ndani ya Shirka la Posta. Waziri amemwaagiza Kaimu Postamasta Mkuu Hassan Mwang’ombe kufuatilia utendaji wa kila idara na kupata taarifa za mara kwa mara ili kuimarisha utendaji wa shirika.

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Posta alimshukuru Waziri Mhe. Mbarawa kwa kutembelea Shirika la Posta na kuahidi kuwa maagizo yote na maelekezo aliyoyatoa atayasimamia kikamilifu ili kuleta tija na Ufanisi zaidi.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: