Friday, 13 April 2018

Watumishi 434 wachukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu


WATUMISHI 434 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria baada ya kubainika kuwa wamezisababishia Halmashauri zao hasara kutokana ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo ya CAG kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka jana.

Jafo alisema hadi Novemba mwaka jana, Ofisi yake ilifanya ufuatiliaji na kujiridhisha kuwa maelekezo yote yalitekelezwa ipasavyo na watumishi hao 434 walichukuliwa hatua.

Alisema hatua hizo zilifuatia hasara zilizosababishwa, hoja za ukaguzi zisizo za lazima kutokana na kutotekeleza ipasavyo wajibu wao au kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu.

Alifafanua kuwa watumishi tisa walifukuzwa kazi, 28 kusimamishwa kazi, 210 kupewa barua za onyo, 15 kufikishwa kwenye vyombo vya dola na 13 wametakiwa kufidia hasara kutoka kwenye mishahara yao.

Wengine ni watumishi wanne wameshushwa vyeo, alisema Jafo, 10 walibadilishwa majukumu, na 64 wapo katika mchakato wa hatua za kinidhamu unaoendelea.

Waziri Jafo alisema mapendekezo ya ukaguzi ambayo hayajafanyiwa kazi katika Halmashauri yamepungua kutoka 3,650 sawa na asilimia 32 ya mapendekezo yaliyotolewa mwaka wa fedha 2014/15 hadi 3,206 sawa na asilimia 25 kwa mwaka 2015/16.

Aidha, Jafo alisema serikali inakubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na CAG kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa ziwe zinapata fedha za ruzuku kwa matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa wakati na kwa kiasi kilichoidhinishwa ili kutoa huduma bora.

Hata hivyo, alisema utekelezaji wa mipango na bajeti ya serikali hutegemea makusanyo halisi ya mapato kutoka vyanzo mbalimbali na kinachotumwa kwenye Mamlaka hizo kinategemea mwenendo wa mapato yaliyopatikana.

“Fedha za miradi ya mendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17 zilizopokelewa ni Sh. bilioni 705.927 sawa na asilimia 57 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Sh. trilioni 1.24,” alisema.

MWONGOZO UNUNUZIAlifafanua kuwa kwa mwaka wa fedha uliotangulia wa 2015/16 fedha za maendeleo zilizopokelewa na Mamlaka hiyo zilikuwa Sh. bilioni 390.5 sawa na asilimia 39 ya bajeti ya Sh. trilioni 1.01.

Akizungumzia kuhusu mapato ya Sh. bilioni 3.53 yaliyokusanywa na Mawakala kutowasilishwa kwa Mamlaka za serikali za mitaa, Jafo alisema kutokana na changamoto hiyo iliyobainishwa na CAG, Tamisemi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeandaa mwongozo wa ununuzi wa huduma ya uwakala wa ukusanyaji mapato kwa mamlaka hizo kwa mwaka 2016.

Alisema lengo ni kuziongoza Halmashauri katika kupata mawakala wenye sifa stahiki na kwamba Ofisi yake imepokea mapendekeo ya CAG kuhusu hilo.

Jafo alisema kiasi cha makusanyo ambacho mawakala hawakukiwasilisha Halmashauri kimepungua hata hivyo kutoka Sh. bilioni 6.03 kwa mwaka 2015/16 hadi Sh. bilioni 3.5 kwa mwaka 2016/17.

Aidha, Jafo aliagiza Halmashauri husika kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinawasilishwa mara moja na haitasita kuchukua hatua kwa wakurugenzi watakaobainika kuzembea kukusanya mapato ya Halmashauri.

Kuhusu udhaifu katika usimamizi wa rasilimali watu na udhibiti wa mishahara, Jafo alisema wizara yake inakubaliana na ushauri wa CAG wa kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi kwa wakati.

Alisema hadi Februari, mwaka huu serikali imelipa sehemu ya malimbikizo ya mishahara kwa walimu na watumishi wengine kiasi cha Sh. bilioni 27.60

No comments:

Post a Comment