Takriban watu 257 wamefariki baada ya ndege ya kijeshi kuanguka kaskazini mwa Algeria , kulingana na wizara ya ulinzi.

Kisa hicho kilitokea muda mfupi baada ya ndege hiyo kupaa kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Boufariki karibu na mji mkuu wa Algiers asubuhi.

Wengi wa waliouawa ni wanajeshi na familia zao kulingana na wizara ya ulinzi huku wafanyikazi 10 wa ndege hiyo pia wakifariki.

Haijulikani ni nini haswa chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo. Afisa mkuu wa jeshi ameagiza uchunguzi wa ndege hiyo na atatembelea eneo la mkasa.

Ni mkasa mbaya wa ndege kuwahi kutokea tangu mwezi Julai 2014 wakati ambapo watu 298 waliokuwa wakiabiri ndege ya Malaysia MH17 walipofariki baada ya ndege hiyo kutunguliwa katika anga ya mashariki mwa Ukraine.

Pia ni mkasa mbaya wa ndege kuanguka tangu 2003.

Mamlaka inajaribu kutafuta mabaki ya waliouawa. Picha kutoka eneo hilo zinaonyesha moshi ukifuka kutoka kwa vifusi vya mabaki ya ndege hiyo.

Ndege hiyo ya Ilyushin Il-76 ilikuwa ikielekea Bachar Kusini magharibi mwa taifa hilo.

Miongoni mwa waliofariki ni wanachama 26 wa chama cha Polisario Front wanaotaka kujitenga kutoka kwa Morocco wa magharibi mwa sahara wanaoungwa mkono na Algeria.

Miaka minne iliopita ndege iliokuwa ikiwabeba wanajeshi na familia zao ilianguka nchini Algeria na kuwaua watu 77.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: