WATOTO wawili waliokuwa wakielekea msikitini, wamefariki papo hapo baada ya kugongwa na basi la kampuni ya Frester katika kitongoji cha Katongo, kijiji cha Rulanda, wilayani hapa, mkoani Kagera.

Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Rais John Magufuli kuwasisitizia madereva kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Augustine Ollomi, alisema jana ajali hiyo ilitokea juzi asubuhi iliyosababishwa na basi lenye namba za usajili T720 EEV lililokuwa kwenye mwendo kasi.

Mtendaji wa Kata ya Rulanda, Adam Kamyani, alitaja majina ya watoto waliofariki kuwa ni Muhajiri Abdumajid (6) mkazi wa kata ya Gwanseli na Abdallah Khalid (7) mkazi wa kata ya Rulanda.

Kamanda Ollomi alisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Mohamed Jafari (49) na hufanya safari zake Bukoba na Mwanza, Alisema baada ya basi hilo kuwagonga watoto hao, lilipinduka na kusababisha abiria 20 kujeruhiwa.

Kamanda Ollomi alisema imekuwa tabia kwa baadhi ya madereva wa maeneo hayo ambayo hakuna askari wa usalama barabarani kuvunja sheria kwa kukimbiza magari ovyo.

“Madereva wetu wamejizoesha lazima washurutishwe kutii sheria, wanapoona trafiki ndipo wanapunguza mwendo, barabara yenye kilomita 100 huwezi kuweka trafiki kila sehemu, madereva watambue wajibu wao wahakikishe wanapoendesha vyombo hivi wanakuwa salama wao, abiria na watumia barabara,” alisema.

Juzi, wakati Rais Magufuli akizindua barabara kuu ya Kaskazini kutoka Dodoma hadi Babati alisema, “Barabara zinapojengwa zinakuwa chanzo cha ajali badala ya kufurahi kuwa na barabara nzuri.

“Barabara zimekuwa chanzo cha kupeleka vilio miongoni mwa Watanzania, tunajukumu kubwa la kuzitumia kulingana na sheria zinavyosema, madereva wanapoendesha wajue wamebeba watu,” alisema.

Aidha, alivitaka kwa mara nyingine vyombo vya ulinzi na usalama vizingatie sheria na kusimamia maadili ya udereva ili kupunguza vilio vya watu vinavyotokana na ajali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: