TUTAKE tusitake, kati ya mwanaume na mwanamke ambaye anatakiwa kuwa makini wakati wa kuchagua mwenza wa kuzaa naye ni mwanamke.

Kwa bahati mbaya wanawake wengi hawalipi uzito mkubwa suala hilo, jambo linalosababisha kuwasumbua watoto baada ya kuzaliwa na wanaume wasiokuwa sahihi. Wiki iliyopita tumeshuhudia wanawake wakipanga misururu kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakilalamika kuhusu wanaume kuwatelekeza watoto wao.

Wengine kabla ya zoezi hilo tulishuhudia wakifikisha matatizo yao katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Ukweli ni kwamba, wanawake wenye busara hawakubali kuzaa au kuolewa kwa kuiga bali kwa kuangalia maisha yajayo. Imekuwa kawaida siku hizi wanawake kuchagua wanaume wa kuzaa nao, wengine kutokana na kipato cha wanaume hao na kusahau kuwa kuzaa ndiyo mwanzo wa familia hivyo unatakiwa kuwa na mtu aliye tayari kwa ajili ya kusaidiana kuhudumia familia.

Ni kweli wapo wanaume wachache ambao wana tabia za ajabu ikiwamo kuendekeza anasa, wanawake na ulevi wa kupitiliza na hawa mara nyingine ndio hujikuta wakizaa na wanamke wasiowatarajiwa. Makosa wanayofanywa ya uchaguzi wanawake wengi huwatokea puani mara tu baada ya kubeba ujauzito au kuzaa, kwa sababu wanaume wa aina hiyo hawapo kwa ajili ya shida wala hawana mpango na familia.

Matokeo yake kina mama huwalea watoto huku wakiwaeleza madhara na kadhia wanayopata kutokana na kutelekezwa na baba zao, jambo ambalo huwaathiri kisaikolojia na kuwapa wakati mgumu kuamua nani kati ya wazazi hao wawili ni sahihi kwao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba anasema siyo vema wazazi kuwahusisha watoto katika makosa waliyofanya wakati wa kuchagua wenza wa kuzaa nao kwa sababu hubaki katika kumbukumbu zao. Anautaja unyanyasaji unaotokana na wazazi kutofanya maamuzi sahihi wanapochagua wenza, ikiwamo vipigo, kutelekezwa na kudharauliwa, mambo ambayo watoto huyaona na kuwajengea chuki mioyoni mwao.

“Unyanyasaji wa aina yoyote haufai kwa binadamu, lakini inapopatikana nafasi ya kufanya maamuzi sahihi kwa namna yoyote ile yafanyike na iwapo kutatokea kutoelewana kwa wazazi, watoto wasiwe sehemu ya ugomvi na misuguano,” anasema mama huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria. Mtaalamu wa Saikolojia na Uhusiano na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki anasema hakuna madhara ya kiafya anayoweza kupata mtoto, lakini inaweza kumtokea mzazi.

“Ni kweli kabisa malezi ya mzazi mmoja wakati wote ni yenye changamoto kwa mzazi mwenyewe. Utafiti ulioandikwa katika moja ya makala za afya ya jamii umeonyesha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wanawake wanaolea watoto pasipo waume zao kupata changamoto za kiafya na kisaikolojia.

“Ingawa changamoto hizi zinaweza kutofautiana kutokana na maeneo au mazingira ya maisha wanayoishi. Baadhi ya changamoto hizi ni kama vile magonjwa na matatizo ya afya ya akili ambayo yana uwezekano mkubwa wa kusababisha ugonjwa wa sonona,” anasema Dk. Mauki.

Anasema katika utafiti huo wanawake 25,000 kutoka nchi tofauti duniani waliulizwa maswali tofauti yakiwemo maswali yahusuyo hali ya ndoa zao, hali za watoto wao na changamoto za malezi wanazokumbana nazo kila siku, sababu zinazokwamisha utendaji kazi wao wa kila siku. Wanawake hawa waliulizwa pia kuhusu hali za afya zao. Kufuatia utafiti huo ilibainika kuwapo kwa uhusiano mkubwa baina ya malezi ya mzazi mmoja wa kike na kuongezeka kwa matatizo ya kiafya na kisaikolojia ukilinganisha na wanawake wanaowalea watoto wao wakisaidiana na waume waliozaa nao.

Wanawake walioonyesha kuwa kwenye hatari kubwa ni wale walioanza malezi ya mzazi mmoja mapema zaidi, hususan wakiwa katika umri wa miaka 20 au chini ya miaka 20. “Wengine ni wale walioendelea kulea watoto peke yao kwa zaidi ya miaka minane na wale wanaolea watoto wawili au zaidi ya wawili wakiwa peke yao, hapa namaanisha pasipo uwepo wa mzazi wa kiume.

“Ukubwa wa matatizo haya umeonekana kutofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa mfano, uhusiano baina ya malezi ya mzazi mmoja na matatizo ya kiafya na kisaikolojia yameonekana kuleta athari kidogo zaidi kwa wanawake wa nchi za Ulaya tofauti na wanawake wa nchi nyingine. Hali ilionekana kuwa mbaya zaidi kwa wanawake wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, nchi zinazoendelea au nyingi zilizo maskini, ikiwamo Tanzania,” alisema.

Mtaalamu Bella De Paulo ambaye ni daktari wa falsafa amesema kuwa baadhi ya wanawake wanaolea watoto peke yao wanaumizwa au kusumbuliwa na ule unyanyapaa kwamba ameachika, ameshindwa kuishi na mume, hajaolewa, alizaa kabla ya ndoa, watoto wake wameharibika, atawezaje kulea mwenyewe? Na maswali yanayofanana na hayo.

Hata hivyo Bella anasema wapo wanawake wachache walioweza kustahimili na kuishi wakiwa na furaha ya kuwapa watoto wao. Anasema miongoni mwa wazazi wa kike wanaolea watoto wao peke yao ni wale waliofanya maamuzi kwa kukurupuka badala ya kufanya uchaguzi sahihi.

Anasema baada ya kuharibu huko nyuma, hutaka kuhusisha watoto kama njia ya kupoza machungu yao bila kujua kuwa wanawaharibu watoto wao kisaikolojia.

“Watoto wadogo kutambua tofauti zilizopo za wazazi wao kwa kusikia au kuona zinaharibu saikolojia yao, hivyo kuathiri maisha yao baadaye,” anasema, hivyo kushauri kushughulikia migogoro hiyo bila kuwahusisha.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: