Jinamizi la ajali limeendelea kuangamiza wanafunzi katika nchi nyingine duniani, ambapo takriban wanafunzi 23 wenye umri wa miaka 4 – 12, wamefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Jumatatu ya Aprili 9, 2018, baada ya basi lao kuacha njia.

Ajali hiyo imetokea nchini India ambapo basi hilo lililokuwa likisafirisha wanafunzi wa shule binafsi ya Wazir Ram Singh Pathania kuelekea nyumbani, kuacha njia na kuserereka katika eneo la Wilaya ya Kangra huko Himachal Pradesh, kwa mujibu wa polisi nchini India.

Jumla ya miili 27 ya watu wakiwemo dereva wa basi hilo, wafanyakazi wawili wa shule hiyo na mwanamke mmoja imeondolewa sehemu ya tukio, na wanafunzi wengine 11 wamekimbizwa hospitali kutokana na kuwa na hali mbaya waliyonayo baadhi yao, huku ikihofiwa kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezaka kutokana na hali walizonazo majeruhi.

Rais wa nchi hiyo Ram Nath Kovind amesema tukio hilo limemuhuzunisha na kutoa pole kwa familia na shule iliyofikwa na misiba hiyo ambayo imeacha baadhi ya familia zikiwa na majonzi makubwa, na kwamba familia hizo zitapatiwa pesa za India rupee lakh 5, ambazo ni zaidi ya milioni 17 za kitanzania kuwapa pole na kuwafariji.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Mei, 2016 ilitokea ajali mbaya nchini Tanzania ambayo iliuwa wanafunzi zaidi ya 30 wa shule ya Lucky Vicent ya mkoani Arusha.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: