Wafanyakazi  watatu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), akiwamo Masoud Kova (36) na wenzao, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kughushi.

Mashtaka mengine ni kujipatia fedha na kuisababishia TPA hasara ya Dola za Marekani 15,618.76 (Sh. 26,041,782.73) baada ya kupitisha kontena 16 bila kulipa ushuru.

Mbali na Kova, washtakiwa wengine ni Lydia Kimaro (52), Ally Mkango (54), Aron Lusingu (35) na wafanyakazi wa Benki ya CRDB, Grace Komba (41) na Juma Ng 'oka (41).

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanaamina Kombakono akisaidiana na Inspekta wa Polisi, Hamis Said.

Katika shtaka la kwanza na la pili, Kombakono alidai kuwa yanawakabili Kimaro na Kova kwamba kati ya Agosti na Septemba, 2014 walitoa taarifa ya uongo kuonyesha kwamba TPA imepitisha nyaraka za malipo ya Dola za Marekani 15,618.76 (Sh. 26,041,782.73) kwa kampuni ya Freight Forwarders (T) Ltd.

Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa kati ya Septemba na Oktoba, 2014, jijini Dar es Salaam washtakiwa wote sita walijipatia dola hizo baada ya kudanganya kuwa fedha hizo ni malipo ya ushuru wa bandari kupitia akaunti ya TPA iliyopo benki ya CRDB.

Shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Septemba na Oktoba, 2014 mshtakiwa Mkango na Lusingu wakiwa waajiriwa wa TPA walishindwa kuzuia kufanyika kosa na kusababisha kampuni ya Freight Forwarders (T) Ltd kupitisha kontena 16 bila kulipa ushuru wa dola hizo.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la tano, kati ya Septemba na Oktoba, 2014 jijini Dar es Salaam, kwa pamoja washtakiwa wote sita waliisababishia hasara hiyo TPA.

Washtakiwa walikana mashtaka yote na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka amewasilisha kibali cha kesi hiyo kusikilizwa na Mahakama ya Kisutu, haukuwa na pingamizi la dhamana.

Hakimu Simba aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili na mmoja kati yao awasilishe Sh. milioni 2.2 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha.

Alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 25, mwaka huu na washtakiwa walitimiza masharti ya dhamana.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: