Halmashauri ya wilaya ya Kasulu iliyopo katika mkoa wa Kigoma inakabiliwa na wimbi kubwa la wagonjwa kutokana na halmashauri za jirani kukosa hospitali, hivyo kufanya Vituo vya afya na Zahanati kushidwa kutoa huduma stahiki, jambo linalosababisha wengi kukimbilia huduma za matibabu katika hosipitali hiyo ya Kasulu.

Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya Kasulu, Dk. Mshana Dastan alisema kuna vituo viwili vya afya vinavyotoa huduma ya upasuaji kwa dharula kwa mama na mtoto, hali inayosababisha hospitali hiyo ya wilaya kujikuta ikikabiliwa na mlundikana wa wagonjwa wanaotoka katika wilaya za jirani ambazo zina vituo vichache vya afya na havitoi huduma ya upasuaji wa dharula.

“Halmashauri za jirani kama Buhigwe na Kasulu mji hazina hospitali, matokeo yake kuna vichache vya afya na haviwezi kukidhi mahitaji ya wagonjwa, hatima yake wengi wanalazimika ama kwa kupewa rufaa au kuja wenyewe katika hospitali yetu kwa ajili ya kupatiwa matibabu,” alisema Dk. Dastan.

Uchache wa vituo vya afya kwenye halmashauri ya Buhigwe na Kasulu mji ndio chanzo kikubwa cha halmashauri ya wilaya Kasulu kujikuta katika wakati mgumu na kutoa huduma kwa watu wengi kutoka nje ya wilaya, ambapo aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kuanza mchakato wa kujenga hospitali za wilaya kwenye halmashauri hizo ili kuwapunguzia adha wananchi.

Alisema utoaji wa huduma ya upasuaji wa dharula kwa kinamama wanaojifungua katika hospitali ya wilaya ya Kasulu inazidi kuzorota kutokana na wanaohitaji huduma kuongezeka na idadi imekuwa kubwa kuliko uwezo wa watoa huduma waliopo katika hospitali hiyo, jambo linaloweza kusababisha ongezeko la vifo vya kinamama na watoto wachanga.

Dk. Dastan alitaja changamoto ya ubovu na uchakavu wa miundobinu ya majengo, vifaa tiba na vitendanishi, upungufu wa wataalamu na watoa huduma wa afya kama mojawapo ya vikwazo vinavyochangia upatikanaji wa huduma zisizokuwa na ubora katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya katika halmashauri hiyo.

“Sera ya afya inaelekeza kwamba kila kata lazima iwe na Kituo cha Afya kinachotoa huduma ya upasuaji wa dharula mkubwa na mdogo na kila kijiji kiwe na Zahanati, lakini sekta ya Afya kwa muda mrefu sasa inakabiliwa na changamoto nyingi hasa upungufu wa vifaa tiba na watumishi ambao ni muhimu wawepo kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa,” alisema Dk Dastan.

Meneja wa Shirika la Engender Health mkoa wa Kigoma, Wilfred Mongo alisema shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya afya wamekuwa wakisaidia kujenga vyumba vya upasuaji, wodi za kinamama na watoto pamoja na kutoa vifaa tiba na vitendanishi, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na hata kuajiri wahudumu wa afya ili wasaidiane na wataalamu kutoa tiba kwa wagonjwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: