Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema serikali imefanikiwa kudhibiti vitendo ya ujangili hapa nchini kwa zaidi ya asilimia 50.

Amesema hayo jana wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma. Mazungumzo hayo yalilenga kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya uhifadhi na maendeleo ya utalii.
Dk. Kigwangalla alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa na kwamba nyara zinazokamatwa hivi sasa ikiwemo meno ya tembo na ngozi za wanyamapori ni masalia ya zamani.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kudhibiti vitendo vya ujangili ikiwemo doria za mara kwa mara za kiitelijensia ambazo zimekuwa zikishirikisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama pamoja na raia wema.
Kwa upande wake balozi Cooke alisema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kudhibiti mtandao wa uhalifu wa madawa ya kulevya, rushwa na ujangili.
Alisema kwa sasa watalii zaidi ya 75,000 wa Uingereza hutembelea Tanzania kila mwaka na wengine wamewekeza katika sekta utalii hapa nchini, hivyo akaiomba Serikali kurekebisha baadhi ya changamoto chache zilizopo katika sekta hiyo kwenye mtiririko wa kodi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: