Na Fatma Salum-MAELEZO
Serikali imekutana na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi wenye nia ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini kwa lengo la kujadili namna ya kufanikisha mchakato huo.

Mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam uliandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kufuatia agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kupata wawekezaji watakaojenga viwanda hivyo.

Akizungumza na wafanyabiashara pamoja na wadau waliohudhuria mkutano huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu alisema kuwa Serikali imeharakisha mchakato wa kuanzisha viwanda vya dawa kutokana na changamoto zilizopo kwenye ununuzi wa dawa nje ya nchi.

“Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inakumbana na changamoto kadhaa katika uagizaji wa dawa nje ya nchi ikiwemo kuletewa dawa baada ya muda mrefu tangu kuagiza, kupungua kwa thamani ya fedha zetu kwa kubadilisha na dola za kimarekani pamoja na kuagiza dawa nyingi kwa mkupuo ambazo hatimaye huharibika kutokana na kukaa muda mrefu,” alisema Ummy.

Pia Waziri Ummy alibainisha kuwa ni muhimu kuanzisha viwanda vya dawa hapa nchini kwani bado watanzania wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

“Mahitaji ya dawa nchini ni makubwa na mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 269 kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba hivyo ni muhimu kujenga viwanda ili fedha za Tanzania ziendelee kuzunguka hapa hapa nchini,” alisema Ummy.

Katika mkutano huo wawekezaji 38wenye nia ya kujenga viwanda hivyo walijitokeza na Waziri Ummy aliwahakikishia kuwa Serikali itanunua dawa za ndani lakini lazima ziwe na ubora na pia viwanda vishirikiane na Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) ili kuhakikisha ubora wa dawa hizo.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda ,Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage aliipongeza sekta binafsi nchini kwa kushirikiana vizuri na Serikali na kukubali kuhudhuria mkutano huo ili kufanikisha azma ya ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.  

“Hili tunalolifanya leo lipo kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ila tunaharakisha mchakato huu ili ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 50 ya dawa tunazotumia ziwe zinazalishwa hapa nchini,” alisisitiza Mwijage.

Aidha alisema kuwa lengo la Serikali ni kutengeneza sekta binafsi imara na kuwataka wadau katika sekta hiyo wajiandae kujenga viwanda vya dawa na Serikali na Taasisi zake zipo tayari kuwasaidia kufanikisha zoezi hilo.

Mkutano huo wa Serikali na wawekezaji wenye nia ya kujenga viwanda vya dawa ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa hapa nchini na Taasisi za Serikali zinazohusika na sekta ya afya zikiwemo Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (MUHAS), Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: