SERIKALI imeagiza kufanyike uchunguzi kuhusu mauaji ya kijana Abdallah Abdulrahman, muuzaji wa matunda mkoani Mtwara anayedaiwa kuuawa na Jeshi la Polisi.

Pia imeagiza kufanyika uchunguzi kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa Jeshi la Polisi wilaya ya Kilwa mkoani Lindi kuua, kutoboa jicho na kunyoa ndevu kwa moto watuhumiwa wa uhalifu wilayani humo.

Akijibu hoja mbalimbali zilizoelekezwa kwa wizara yake katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema ameagiza kufanyika uchunguzi wa ndani ili serikali ipate taarifa juu ya matukio hayo.

Waziri huyo pia alisema wataendelea kutoa taarifa zitakazopatikana kutokana na uchunguzi wa matukio hayo.

Lakini, Dk. Mwigulu aliwataka wabunge kuepuka kuyahusisha matukio hayo na itikadi za kidini, kisiasa na kikabila.

“Lakini nimweleze mbunge pale kunapokuwapo na jambo limempata Mtanzania mmoja, tuepuke sana kuliunganisha jambo hilo na dini yake," alisema.

"Yanapotokea matuko ya kiuhalifu, mtu hakamatwi kutokana na dini yake, wala kabila lake wala itikadi yake ya kisiasa, mtu anakamatwa kutokana na kosa lake."

Alisema ingekuwa matukio hayo ya kihalifu hayafanywi na watu wa dini, vyama na makabila yaliyopo, basi kuna mahali pengine ambako wanaamini kuwa ni mahali patakatifu wasingekamata wahalifu.

Ingawa hakumtaja kwa jina, kauli za Dk. Mwigulu zilionekana kumlenga Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala, maarufu kama Bwege (CUF), ambaye juzi alisema bungeni kuwa kuna watu walikamatwa na polisi msikitini na  kurudi uraiani mmoja wao akiwa hana jicho, mwingine amenyolewa ndevu kwa moto na mwingine akiwa marehemu.

Mbunge huyo pia alisema wapo watu wawili ambao anao ushahidi kuwa walichukuliwa na Jeshi la Polisi lakini hawajulikani walipo hadi sasa na kuitaka serikali kusema waliko.

Bwege alikwenda mbali zaidi akieleza kuwa sasa kimbilio la wananchi ni mahakama na maaskofu akidai kuwa viongozi wa waislamu hawatoi waraka wa kulaani matukio ya mauaji nchini wakihofu kubambikiwa kesi za ugaidi.

Katika majibu yake kuhusu hoja hiyo, Dk. Mwigulu alisema wizara yake inafanyia kazi changamoto ya wananchi kubambikiwa kesi ambayo alibainisha kuwa hata Rais John Magufuli ameshaagiza ishughulikiwe ili haki itendeke.

Madai ya kuuawa kwa mvuvi mkoani Mtwara yalitolewa bungeni mjini hapa na Mbunge wa Mtwara, Maftaha Nachuma (CUF), ambaye alisema kijana huyo alipigwa risasi na polisi wakati akiwa katika shughuli zake za uvuvi kwenye fukwe za bahari.

Nachuma aliitaka serikali kuunda tume kuchunguza tukio la mvuvi aliyedai ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi Machi 25 wakati akivua baharini.

Alidai kuwa mvuvi huyo alikuwa anaendelea na shughuli zake baharini lakini ghafla polisi wakiwa na maofisa uvuvi walimtaka kujisalimisha.

"Kutokana na uoga, mvuvi huyo alikimbia ndipo polisi walimpiga risasi maeneo ya kisogoni," alisema.

Katika maelekezo yake kuhusu hoja ya mbunge huyo wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliitaka serikali kulitolea ufafanuzi baadaye kama itaona inafaa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: