Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack

SERIKALI ya Kata ya Nsalala, Tarafa ya Itwangi, mkoani Shinyanga vijijini imetunga sheria ndogo ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni kwa kumtaka mtu yeyote anayetaka kuoa ama kuozesha kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji. Lengo la sheria hiyo ni ili kujiridhisha kuwa anayeolewa siyo mwanafunzi au msichana chini ya umri wa miaka 18.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nsalala, Sandeko Machungo kwenye mkutano maalum wa kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia ndani ya jamii ulioandaliwa na Shirika la Kivulini linalotetea haki za watoto na wanawake kwa ufadhili wa Oxfam la Uingereza.

Alisema viongozi wa kijiji wamepata elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na ndiyo maana wakaona watunge sheria hiyo ndogo kijijini hapo ili kuzuia wananchi kuoa ama kuozesha bila ya kutoa taarifa kwenye uongozi huo kwa lengo la kutokomeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

“Tumeshatunga sheria kijijini hapa kwamba hakuna mwananchi kuoa au kuozesha bila kuuona uongozi wa kijiji, sasa tunafuatilia taarifa za mtu anayetaka kuoa au kuoza ili kuhakikisha wanaoolewa wamefikisha umri wa miaka 18 na kuhakikisha kuwa siyo mwanafunzi kwa kuangalia vyeti vya kuzaliwa ama kadi ya kliniki ndipo tutatoa ruhusa,” alisema Machungo.

Alibainisha kuwa sheria hiyo waliitunga mwaka jana na tayari wananchi wamekuwa wakifanya hivyo na tangu ianze sasa hakuna shangamoto tena za ndoa za utotoni katika eneo lake wala mimba za wanafunzi.

“Kila mwananchi amekuwa mlinzi wa mwenzake na atakayebainika kwenda kinyume cha sheria hii, uongozi wa kijiji utamshughulikia.
Naye Kaimu Afisa wa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Shinyanga Vijijini, Aisha Omari aliipongeza serikali ya kijiji hicho kwa kutunga sheria hiyo ndogo na kutoa wito kwa vijiji vingine nchini kuiga mfano huo ili kutokomeza ndoa na mimba za utotoni
Share To:

msumbanews

Post A Comment: