Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amezindua zoezi la utoaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV) ikihusisha wasichana wenye umri wa Miaka 14.
RC Makonda amesema zoezi hilo litaanza rasmi Jumatatu ya February 23 likihususisha zaidi ya Wasichana 24,097 ambao watakaopata chanjo hiyo katika vituo 270 ikiwemo shule na mitaa.
Aidha RC Makonda amesema utoaji wa chanjo hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ukisababisha vifo vya kinamama wengi huku akiitaka jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.
Pamoja na hayo RC Makonda ametoa wito kwa viongozi wa dini, madiwani, wenyeviti wa mitaa na wajumbe kuhamasisha jamii kwenda kupata chanjo hiyo.
Hata hivyo RC Makonda amesema chanzo cha ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na mapenzi katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuzaa watoto wengi pamoja na uvutaji wa sigara ambapo dalili zake ni kutokwa na damu bila mpangilio, maumivu ya mgongo, miguu, kiuno, kutokwa na uchafu ukeni pamoja na kuchoka, kupungua uzito na hamu ya kula.
RC Makonda amesema Saratani ya mlango wa kizazi inasababishwa na virusi vya Human Papilloma ambapo kinga yake kwa hatua ya mwanzo ni kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini dalili za mwanzo na kupata matibabu stahiki.
Chanjo ya Saratani ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa mwaka 2018 itatolewa kwa wasichana wanaotimiza umri wa miaka 14 ambao wamezaliwa kuanzia January 01 hadi Disemba 31 mwaka 2004.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: