Saturday, 7 April 2018

RC Gambo amtoa hofu Rais Magufuli

  

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho gambo amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutotishwa na mambo ya mitandaoni, kwani mkoa wa Arusha uko salama.


Mrisho Gambo ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salam zake kwa Rais Magufuli, kwenye sherehe za uzinduzi wa nyumba za polisi mkoani Arusha, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abedi.

Kwenye salamu hizo Mrisho Gambo amesema mkoa wa Arusha ni salama na wakazi wa Arusha hawana haja ya maandamano, kwani wanachohitaji ni uongozi wake ambao unawaletea maendeleo makubwa.

Mrisho gambo aliendelea kwa kueleza kuwa anatambua kazi ya kubwa aliyonayo Rais ya kupigana vita ya uchumi, na watu wengi wasiopenda nchi hii watachukia kutokana na hilo.

“Mheshimiwa Rais nikuhakikishie tu Arusha ni salama, wala usitishwe na mbwembwe za kwenye mitandao, watanzania halisi ni hawa hapa wenye Arusha yao. Watanzania wa Arusha wamechoka na maandamano, wanataka uongozi wa kwako ambao unawaletea maendeleo. Ninajua vita uliyokuwa nayo ni kubwa sana, Mwl. Nyerere alikuwa na vita ya ukombozi, akaimaliza salama, Mheshimiwa Rais vita yako wewe ni ya kiuchumi, ni vita inayopigana na mabeberu ambao wanawatumia wengine kukwamisha jitihada zako. Watu wengi ambao hawaitakii mema nchi hii hawawezi kuipenda”, amesema Mrisho Gambo.

Sambamba na hilo Mkuu wa mkoa huyo wa Arusha amemshukuru Rais Magufuli na wadau kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo za askari polisi, ambazo awali ziliteketea kwa moto.

No comments:

Post a comment