Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli akizungumza na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya
Nchi kabla ya kuzindua rasmi Taasisi hiyo isiyo ya Kiserikali ya Jakaya Mrisho
Kikwete(JMKF) Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli akipigiwa makofi mara baada ya kumaliza kusoma hotuba
yake na kuizindua rasmi Taasisi hiyo isiyo ya Kiserikali ya Jakaya Mrisho
Kikwete(JMKF) Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya (JKMF) Rais Mstaafu wa
awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza kabla ya uzinduzi
wa Taasisi hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli akimpongeza Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya (JKMF) Rais
Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya
kuizindua.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya (JKMF)
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya
kuizindua. PICHA NA IKULU
*Azungumzia mambo makubwa ambayo aliyafanya kwenye utawala wake ambayo yatakumbukwa
*Azindua rasmi Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation,aahdi Serikali kutoa ushirikiano mkubwa
*Alezea Kikwete alivyosababisha awe Rais wa Awamu ya Tano, Kikwete azungumzia malengo ya taasisi
Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii.
RAIS
Dk. John Magufuli amesema kwa kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais
mstaafu Jakaya Kikwete kwenye uongozi wake kuna mambo makubwa ya
maendeleo katika nchi yetu huku akitanguliza uzalendo mkubwa Watanzania
wanamkumbuka na wataendelea kukumbuka watake wasitake.
Pia ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa Rais mstaafu Kikwete kwani ndio amesababisha awe Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano huku akitumia nafasi hiyo kuahidi kuwa atahakikisha
Serikali yake itashirikana na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete
inayofahamika kwa Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF)ambayo
ameizindua rasmi leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
"Mzee wangu Kikwete naomba niseme kutoka moyoni wakati wa uongozi wako umefanya mambo makubwa
ya kuleta maendeleo kwa ajili ya nchi yetu ya Tanzanania.Kuna miradi
mikubwa ya maendeleo ambayo ameifanya na imeacha alama ambayo itatufanya
watanzania tumkumbuke.Kwa kazi ambayo umeifanya kwa uzalendo mkubwa
ndani ya nchi yetu Watanzania tunakukumbuka na tutaendelea kukumbuka
watake wasitake,"amesema Rais Dk.Magufuli.
Ametaja ipo mifano mingi hai ya mambo ambayo ameyafanya Rais mstaafu Kikwete kwenye Serikali ya
Awamu ya nne na baadhi ya miradi hiyo lipo la ujenzi wa bomba la gesi
kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam, ujenzi wa miundombinu ya
barabara nchi nzima, ujenzi wa miradi ya maji , umeme na kuimarisha
sekta muhimu za afya, kilimo na vijana.
"Rais
mstaafu Kikwete alilitumikia Taifa la Tanzania kwa uadilifu
mkubwa.Tabia ya binadamu wamekuwa na kawaida ya kumsifu mtu baada ya
kufa na kusema pengo halitazibika wakati si kweli kwani kama ni nafasi
ya uongozi inaweza kujazwa wakati huohuo.Kwa Rais mstaafu na mzee wangu
Kikwete naomba nikusifu ukiwa hai tena upo mbele yangu
unatabasamu.Umefanya kazi kubwa ya kizalendo kwa ajili ya nchi yetu ya
Tanzania na unastahili sifa na shukrani kutokana na mchango wao wa
kuleta maendeleo kwenye nafasi mbalimbali.
"Ulipokuwa
Rais wa Tanzania umefanya mambo makubwa zaidi kwa ajili ya nchi yetu.
Katika utawala wako umefanikisha ujenzi wa shule za sekondari za kata ,
ujenzi wa Hospitali ya Mloganzila na miradi mingine mikubwa ambayo
umeifanya na sote ni mashahidi kwa yale ambayo umeyafanya,"amesisitiza
Rais Dk.Magufuli na kuongeza mbali ya kuwa Rais mzee Kikwete ameshika
nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Bara la Afrika na nchi za ulaya na
Dunia kwa ujumla na kote huko ametoa mchango mkubwa wa kuleta maendeleo
.
Rais
Magufuli amesema uzalendo wa mzee Kikwete kwa nchi yake umemfanya hata
baada ya kustaafu kuamua kuanzisha taasisi ambayo leo amezindua rasmi na
vipaumbele vya taasisi hiyo havina tofauti na vile ambavyo
anavitekeleza kwenye Serikali yake , hivyo ameahidi kumpa ushirikiana
mkubwa kufanikisha malengo hayo na kuomba wadau wengine wakiwamo
mabalozi nao kuunga mkono kazi za taasisi hiyo.
"Mzee
Kikwete ameiga mfano wa watangulizi wake kuanzia Mwalim Nyerere, Mzee
Mwinyi na mzee Mkapa ambao nao baada ya kustaafu kuongoza nchi waliamua
kuendelea kutoa mchango wao wa kulitumikia taifa na hivyo kitendo cha
Rais mstaafu Kikwete kuanzisha taasisi hiyo imeonesha uzalendo na
utayari wake wa kuendelea kutoa mchango wake kwa nchi yake na Bara la
Afrika kwa ujumla kwani taasisi hiyo itatoa huduma zake ndani na nje ya
nchi yetu,"amesema.
AZUNGUMZIA VIPAUMBELE VYA TAASISI
Rais
Dk.Magufuli ameeleza namna ambavyo amefurahishwa na vipaumbele vyake
katika kuwatumikia Watanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.Amefafanua
kuna vipaumbele vinne na kipaumbele cha kwanza ni eneo la afya na
Watanzania wanafahamu umuhimu wa eneo la afya kwani ili nchi iwe na
maendeleo lazima watu wake wawe na afya njema.
Amesema Serikali yake imeendelea na jitihada za kuhakikisha inapunguza vifo kwa mama mjazito na watoto
chini ya miaka mitano na kufafanua kuwa Rais mstaafu Kikwete akiwa
madarakani alifanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto
wenye umri chini ya miaka mitano.
"Nimefurahi
kuona suala la afya limepewa kipaumbele kwenye taasisi hii mpya ambayo
naizindua leo hii. Nami kwenye Serikali nimeendelea kuboresha vituo vya
afya na sasa tunaendelea na upanuzi wa vituo vya afya 170 ambapo lengo
viwe vinafanya upasuaji kwa mama wajawazito ili kuokoa
maisha,"amesema Rais Dk Magufuli na kuongeza wanaendelea na kutoa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano na lengo ni kupunguza vifo,"amesema.
Amesema kipaumbele cha pili ni vijana na kueleza kuwa kuna changamoto nyingi katika kundi hilo ambalo linahitaji kusaidiwa na taasisi ya Rais mstaafu Kikwete imeamua kuelekeza nguvu zake wakati
kipaumbele cha tatu ni sekta ya kilimo na kwa Tanzania sehemu kubwa ya
watu wake wamejikita kwenye sekta hiyo.Kipaumbele cha nne ni utawala
bora na amani na kufafanua nalo ni eneo muhimu na kueleza vipaumbele
vyote hivyo navyo ndivyo vipaumbele vyake na hata kwa nchi nyingine za
Afrika.
"Taasisi
hii imeahidi kushirikiana na Serikali na si kushindana.Hivyo
tutahakikisha tunashirikiana nayo kwa karibu na nieleze tu sitakuwa
tayari kushirikiana na taasisi yenye lengo la kuvuruga amani ya nchi na
ninakushukuru mzee Kikwete umeeleza wazi namna ambavyo utashirikiana
nasi,"amesisitiza.
Rais Magufuli ameeleza namna ambavyo anamshukuru Rais mstaafu Kikwete na kufafanua hata yeye kuwa
Rais imetokana na yeye na huo ndio ukweli, hivyo popote atakapomuana
ataendelea kumshukuru. Pia amewashukuru viongozi wengine wa ngazi
mbalimbali na anafurahia kuona wapo marais wastaafu wamemzunguka na
kumpa ushauri na maelekezo yanayomsaidia kutekeleza majukumu yake.
KIKWETE AMSHUKURU DK MAGULI, AZUNGUMZIA TAASISI YAKE
Kwa upande wake Rais Mstaafu Kikwete amesema kuwa anamshukuru Rais Magufuli kwa kukubali kuzindua taasisi hiyo na kuipa heshima ya hali ya juu na kutumia nafasi hiyo kuahidi kuwa lengo la kuanzishwa
kwa taasisi hiyo ni kufanya kazi katika maeneo ambayo wameamua kuanza
nayo zaidi kama sehemu ya kutoa mchango wao katika kushirikiana na
Serikali kutekeleza majukumu yake.
Amefafanua
wakati anakaelekea kustaafu , alianza kufikiria akiwa na wasaidizi wake
nini afanye baada ya kustaafu na hivyo walikubaliana mambo mawili, moja
kuanzisha taasisi hiyo na mbili kuandika kitabu ambacho nacho
atakifanikisha.
Amelezea maeneo ambayo wamekubaliana na bodi ya wadhamini wa taasisi hiyo ya kuanza nayo na kufafanua
wanatambua yapo maeneo mengi lakini wameanza na mambo manne likiwemo
eneo la afya ya mama mjazito na mtoto."Ni falsafa na sera ya msingi kuwa
tutafanya kazi kwa karibu na Serikali na hakuna sababu ya kusigana na
Serikali na hatutakubali kushawishiwa na mtu yoyote."
Ameongeza Serikali ndio washirika namba moja na kueleza kuwa hivyo wao wanachokifanya ni kuendelea
kusaidia kazi inayofanywa na Rais Dk.Magufuli na nchi nyingine za
Afrika.Shabaha yao ni kwamba pale ambao wengine wapo wao hawatakwenda na
hata wakienda basi ni kuongeza nguvu na kubwa zaidi hakuna
wanayeshindana naye.
"Nakushukuru Rais kwa moyo wako wa upendo kwangu na Watanzania kwa ujumla na kwamba kazi kubwa ya kuleta maendeleo ambayo unaifanya sote tunaiona.Natambua kunachangamoto nyingi ambazo unakabiliana nazo lakini tutaendelea kukuombea kwa Mungu ili utekeleze vema majukumu
yako,"amesema Rais mstaafu Kikwete.
Post A Comment: