RAIS Dk. John Magufuli  anatarajia kuzindua rasmi  Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete inayofahamika kwa Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete ulioko Ikulu, Dar Es Salaam.

Rais mstaafu Kikwete ndiye Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya JMKF na uzinduzi huo rasmi utahusisha maofisa waandamizi wa Serikali, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania na hasa mabalozi wa Afrika ambako Taasisi hiyo inalenga kufanya kazi mbali ya Tanzania, wakuu wa taasisi mbali mbali za kimataifa, wadau wa Taasisi ya JMKF, wakuu wa asasi zisizokuwa za kiserikali (NGO’s) na wakuu wa taasisi za kijamii wakiwemo viongozi wa dini.

Taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Pioneer Communications Limited kwa niaba ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF)imesema uzinduzi huo  utafuatiwa na chakula cha jioni ambacho Rais Magufuli atawaandalia wageni watakaohudhuria sherehe hiyo ya uzinduzi, akiwemo Rais Kikwete mwenyewe na mkewa Mama Salma Kikwete.

"Taasisi ya JMKF iliyosajiliwa rasmi mwanzoni mwa mwaka Februari, 2017, ilianza kazi Machi, mwaka jana wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi ya Wadhamini ya Kimataifa ya Taasisi hiyo ilipofanya kikao chake kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Hyatt mjini Dar Es Salaam,"imesema taarifa hiyo.

Imeongeza taasisi hiyo inayolenga kufanya kazi na kuelekeza nguvu zake katika maeneo matano, itaanzia na maeneo matatu ambayo ni Afya ya Mama na Mtoto, Maendeleo ya Vijana na Uwezeshaji wa Wakulima Wadogo katika maeneo ya vijijini na mashambani katika jitihada zao za kujinasua katika umasikini ama kupunguza athari na madhara ya hali ya umasikini.

"Mheshimiwa Kikwete anasaidiwa katika uendeshaji wa Taasisi hiyo na Bodi ya Wadhamini yenye sura ya Kimataifa ambayo wajumbe wake wanatoka nchi za Tanzania, Marekani, Afrika Kusini, Ureno na Malaysia.Wadhamini hao ni Balozi Ombeni Sefue aliyepata kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Balozi wa Tanzania katika  Canada na Marekani.

"Pia Profesa Rwekaza Mukandala aliyekuwa Makamu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwa miaka mingi, Profesa William Mahalu wa Chuo Kikuu cha Mt. Agustine mjini Mwanza na Balozi Mwanaidi Sinare Majar ambaye amepata kuwa Balozi wa Tanzania katika Uingereza na Marekani,"imefafanua.

Wengine ni Mfanyabiashara maarufu Abubakar Saidi Bakhressa, Balozi Charles R. Stith aliyepata kuwa Balozi wa Marekani katika Tanzania, Msomi na Mtumishi wa Umoja wa Mataifa Bwana Carlos Lopez, Waziri mwandamizi katika Serikali ya Malaysia, Dato Sri Idris Jala na  Mtaalamu wa Masuala ya Fedha kimataifa Genevive Sangudi, Mtanzania mwenye makazi yake Afrika Kusini na Marekani.

Kutokana na kikao hicho cha kwanza cha Bodi ya Udhamini Machi mwaka jana, wataalamu mbali mbali pamoja na washauri wa kila aina, wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa JMKF,  Omari Issa wamekuwa katika matayarisho makubwa ya kuandaa nyaraka mbali mbali za msingi za kuongoza dira na dhima ya Taasisi hiyo kwa ajili ya uzinduzi rasmi na kwamba shughuli hiyo ya Ikulu itatangazwa moja kwa moja kwenye Televisheni ya Taifa ya TBC na vyombo vingine.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: