Rais John Magufuli anatarajiwa kulihutubia Bunge la Afrika Mashariki(Eala) katika mkutano wake wa nne kikao cha kwanza ulioanza leo mjini Dodoma ikiwa ni mara ya kwanza vikao vya bunge hilo kufanyika huko.

Taarifa ya Eala kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisa Habari Mwandamizi, Bobi Odiko ilisema mkutano huo utafanyika kati April 9 hadi 28 mwaka huu na Rais Magufuli atalihutubia katika muda utakaopangwa na taarifa itatolewa wiki ijayo.

Spika wa Bunge hilo, Martin Ngoga ataongoza mkutano huo wa wiki tatu ambao utajadili miswada na maazimio mbalimbali wakati kamati za bunge zimeendelea kuandaa miswada kwa ajili ya mkutano huo.

“Kwasasa ipo miswada miwili itakayojadiliwa kwa kina inayohusu Itifaki ya Sarafu Moja ambayo ni mswada wa taasisi ya Fedha na  mswada wa Takwimu yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  ya mwaka 2017,”alisema Odiko.

Amesema miswada hiyo iliwasilishwa katika bunge hilo na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri  wa EAC, Dk Kirunda Kivenjija na ilishasomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa pili uliofanyika  Januari jijini Kampala.

 Taarifa imesema lengo la mswada wa taasisi ya Fedha ya EAC wa mwaka 2017 unakusudia kuanzisha taasisi ya jumuiya ambayo itakua na majukumu ya kuweka taratibu za kuanza Umoja wa Sarafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.                                      
“Kwa mujibu wa Ibara ya 23 ya Itifaki iliyoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inataja Umoja wa Sarafu ya EAC, hivyo muswada huo unatarajiwa kuweka majukumu, uongozi na namna ya kupata fedha za kuendesha taasisi hiyo,”alisema Odiko. 

Pia muswada wa Takwimu wa EAC wa mwaka 2017 unalenga kuanzisha taasisi ya takwimu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama inavyotajwa kwenye Mkataba wa EAC ibara ya 9 na 21  ya Itifaki iliyoanzisha Umoja wa Sarafu wa EAC
   
Amesema Baraza la Mawaziri wa EAC wanatarajiwa kukutana mapema na kamati mbalimbali za bunge hilo kupitia mambo muhimu ya miswada hiyo huku kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji ikitarajiwa kukutana na wadau juu ya muswada wa Takwimu wa EAC.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: