Jumla ya maofisa wa Jeshi la Polisi wapatao 458 wamefukuzwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu kuanzia mwaka 2015 hadi Machi mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa jana Aprili 7 na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro alipokuwa akizungumza mbele ya Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa nyumba 31 za Polisi na ufunguzi wa kituo cha Polisi cha Utalii na Kidiplomasia jijini Arusha.

Sirro alisema kazi ya Jeshi la Polisi ni kurekebisha mienendo ya wananchi, hivyo kabla hawajawaelimisha wananchi wanapaswa kuwa na mienendo mizuri wao kwanza.

Alifafanua kwa kulitambua hilo ndiyo maana askari waliokwenda kinyume na azma hiyo walichukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, ambapo kwa mwaka 2015, 198 walifukuzwa kazi.

Alisema kwa mwaka 2016 walifukuzwa askari 165, 2017 (81) na kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu wamefukuzwa askari 14.

“Hatuna muhali kuwachukulia hatua askari wanaokiuka utaratibu na nidhamu ya utendaji katika Jeshi la Polisi,” alisema IGP Sirro.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: