SERIKALI ya Kijiji na Kata ya Nsalala Tarafa ya Itwangi Shinyanga Vijijini, imetunga sheria ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, kwa kumtaka mwananchi anayetaka kuoa ama kuozesha kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.

Lengo la marufuku hiyo ni ili kijiridhisha kama anayeolewa siyo mwanafunzi au msishana chini ya umri wa  miaka  18.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nsalala, Sandeko Machungo, kwenye mdahalo wa kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia ndani ya jamii kupitia mitandao ya kijamii, ulioandaliwa na Shirika la Kivulini linalotetea haki za watoto na wanawake kwa ufadhiri wa shirika la OXFAM la Uingereza.

Alisema viongozi wa Serikali ya kijiji mara baada ya kupata elimu ya ukatili wa kijinsia kupitia mashirika mbalimbali, wameona ni vyema wakatunga sheria ndogo kijijini ya kuzuia wananchi kuoa amakuozesha bila ya kutoa taarifa kwenye uongozi huo kwa lengo la kutokomeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

“Kwenye kijiji changu tumetunga sheria, hakuna mwananchi kuoa ama kuozesha bila ya kuuona uongozi wa kijiji, tutafuatilia taarifa za mtu anayetaka kuolewa kama hayupo chini ya umri wa miaka 18 na siyo mwanafunzi, kwa kuangalia cheti cha kuzaliwa ama kadi ya klinini ndipo tunatoa ruhusa,” alisema Machungo.

Aliongeza sheria hiyo waliitunga mwaka jana na wananchi wamekuwa wakifanya hivyo, na tangu ianze kufanyakazi hakuna changamoto tena ya ndoa za utotoni kijiji humo wala mimba kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa Machungo, kila mwananchi amekuwa mlinzi wa mwezake na atakaye bainika kwenda kinyumena sheria hiyo kijiji kitamshughulikia.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: