Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, ametolea ufafanuzi suala lililoibuliwa na Mbunge wa Kilwa Kusini Suleiman Bungara, kuhusu polisi kushambulia watu msikitini na wengine kuuawa.

Akizungumza Bungeni leo Waziri Nchemba amesema kwamba yeye kama waziri mwenye dhamana amelisikia suala hilo na ameagiza uchunguzi ufanyike, ili kuweza kubaini mbivu na mbichi na sheria kufuata mkondo wake.

Sambamba na hilo Waziri Nchemba ameitaka jamii kutohusisha makosa ya uhalifu na masuala ya dini au siasa, kwani mhalifu anapokamatwa hakamatwi kwa imani ya dini au chama chake, bali ni kwa makosa aliyofanya.

“Nimewaelekeza wafanye uchunguzi wa ndani ili tuweze kupata taarifa kamili na tutatoa taarifa, na nimuombe mheshimiwa mbunge tuepuke sana kulinganisha jambo hilo na dini, linapotokea suala la uhalifu mtu hakamatwi kwa dini yake, anakamatwa kwa kosa alilolifanya, watu wanakamatwa kutokana na makosa aliyofanya wala asiunganishwe kwa dini yake au chama chake”, amesema Mwigulu Nchemba.

Hapo jana Mbunge wa kIlwa Kusini Suleiman Bungara maarufu kwa jina la Bwege alimtaka Waziri atolee ufafanuzi suala la polisi kuingia msikitini na kupiga risasi, na kuchukua baadhi ya watu ambao wengine walirudi wakiwa marehemu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: