MUME AMPASUA KICHWA MKEWE KWA SHOKA


Nyumba anayoishi.
DAR ES SALAAM: Ukatili dhidi ya wanawake unaendelea! Siku chache baada ya Mtanzania Leyla Mtumwa kudaiwa kuuawa kwa kuchomwa visu na mumewe, Keme Kasambula jijini London, nchini Uingereza, Mtanzania mwingine Elisha Misefa ‘Rasi’, mkazi wa Mtaa wa Yange Yange, Kata ya Msongola, Ukonga jijini Dar amedaiwa kumpasua kichwa kwa shoka mkewe, Habiba Said na kutokomea kusikojulikana.

Shemeji mtu akionyesha eneo la tukio, kitandani.

NI IJUMAA ILIYOPITA
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Ijumaa iliyopita majira ya saa 4 asubuhi ambapo awali, majirani waliwaona wanandoa hao wakiwa pamoja lakini baadaye walikuja kushtuka kuona mwanamke huyo akiwa amezimia ndani ya chumba wanachoishi huku akiwa amepasuliwa kichwani na damu zikimvuja.

SHEMEJI AFUNGUKA
Akizungumza na Gazeti la Amani, shemeji yake Habiba aitwaye Mbaraka Abdallah, alisema siku hiyo ya tukio, alipewa taarifa na kijana aitwaye Abdallah Hamisi ambaye alikwenda kumtazama Habiba ambaye ni mama yake mdogo na kumkuta akiwa uchi wa mnyama kitandani huku mwili mzima ukiwa umetapakaa damu
“Unajua siku hiyo, shemeji (Habiba) alikuwa anatakiwa akawapokee watoto Stendi ya Mabasi ya Mikoani Ubungo waliokuwa wanatoka Morogoro.
“Sasa alikuwa akiwasiliana na watu wa Morogoro kwenye simu lakini ghafla majira ya saa nne hivi, mawasiliano yalikata wakati wakiwa tayari wameshawapakiza watoto kwenye basi la kuja Dar,” alisema shemeji huyo.

Aliongeza kuwa wale ndugu wa Morogoro walipoona mawasiliano yamekatika ndipo walipolazimika kumtafuta Abdallah ambaye ni mtoto wa dada yake Habiba ili aweze kwenda kumuangalia mama yake mdogo nyumbani kwake kujua kulikoni amekata mawasiliano.

Habiba Said kabla ya kujeruhiwa.

AKUTA MLANGO UMEFUNGWA
Shemeji huyo aliendelea kueleza kuwa, baada ya kijana huyo kufika kwenye chumba cha mama yake mdogo, alikuta mlango umefungwa na alipojaribu kuita, hakuna mtu aliyeitika.

AINGIA NDANI
Shemeji huyo alisema baada ya kuita kwa muda, kijana huyo aliamua kuufungua mlango na ndipo alipomkuta mama yake mdogo akiwa amelala kitandani akiwa amepoteza fahamu na kichwani kuna majeraha makubwa, akamfuata yeye na kumpa taarifa.
“Baada ya kunieleza, nilitoka mimi pamoja na ndugu wengine wa karibu ambapo kweli tulipofika tukamkuta Habiba akiwa ameumia na amezimia, chumba kizima kikitapakaa damu,” alisema shemeji huyo.

Jilani.
 WARIPOTI POLISI
Baada ya kuona Habiba amezimia na ana hali mbaya, ndugu hao walikwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Msongola ambapo walipewa fomu maalum ya matibabu (PF 3), wakamchukua mgonjwa wao na kumpeleka Hospitali ya Mbagala lakini nako walishauriwa wampeleke Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Tulipomfikisha Muhimbili, Habiba alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ambapo hadi leo (Jumatatu iliyopita) ndio tumepata taarifa kuwa amezinduka na kuanza angalau kunywa uji kwa kutumia mrija,” alisema shemeji huyo
Eneo alipokuwa akiuza chakula.
MAFUNDI WALIMUONA MTUHUMIWA
Katika mazungumzo mengine, shemeji huyo alisema baadhi ya mafundi waliokuwa wanajenga katika nyumba za jirani, karibu na nyumba aliyokuwa anaishi Habiba, walimuona Rasi akitoweka huku akiwa na damu kwenye mwili wake na hata walipomuuliza, alisema amepata ajali.
“Kuna mafundi walimuona wakati anaondoka na walipomuuliza kwa nini ana damu kwenye mwili wake, aliwajibu kuwa amepata ajali,” alisema shemeji huyo.

JIRANI NAYE ANENA
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni jirani yake Habiba aitwaye Mariamu Kiburura, alilielezea tukio hilo na kusema liliwashtua kwani hawakutegemea kama lingeweza kufanyika muda wa mchana kweupe.
“Nilitoka kwenye mihangaiko yangu, muda wa saa nane hivi nafikiri ndipo tulisikia kuwa kuna tukio limetokea hapa nyumbani kwa Habiba ndipo tukaenda pale tukaingia ndani na kumkuta akiwa amelala kitandani na mwili wake ukiwa umetapakaa damu, ndio ndugu zake wakamchukua wakapitia polisi na baada ya hapo wakampeleka hospitali.
“Inauma maana tukio limetokea mchana kabisa, tunamuombea kwa Mungu ili aweze kupona ili aendelee na shughuli zake,” alisema shuhuda huyo.

Shoka lililotumika

MWENYEKITI ENEO LA TUKIO
Mwenyekiti wa Mtaa wa Yange Yange, Kata ya Msongola, Ukonga Dar, George Mohele, alipoulizwa na gazeti hili la Amani alikiri kutokea kwa tukio hilo katika eneo lake ambapo aliambata na wanahabari wetu hadi nyumbani hapo na kushuhudia chumba kilichofanyika unyama huo kikiwa kimetapakaa damu.

Mwenyekiti huyo alisema kwa kuwa suala hilo lipo chini ya polisi, wanaliacha jeshi hilo liendelee kufanya uchunguzi wake na kuweza kumweka mtuhumiwa kwenye mikono ya sheria ili ifuate mkondo wake.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamduni, simu yake iliita bila kupokelewa kisha alipopigiwa kwa mara nyingine, alituma ujumbe mfupi akieleza kuwa yupo kwenye kikao. Hata hivyo, baadhi ya maofisa wa polisi ambao waliomba majina yao yasiandikwe gazetini kwa kuwa siyo wasemaji walikiri kutokea kwa tukio hilo.Bonyeza hapa Download Msumbanews kutoka playstore

Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: