Mume aezua paa la nyumba, kisa mkewe kumzalia watoto wa kike


“Aliapa kuwa lazima afanye kitendo hiki kwa sababu mimi sina faida, namzalia watoto wa kike tu,” ni kauli ya Miriam Jackson, mama wa watoto wanne aliowazaa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka 15.

Mwanamke huyo amelazimika kwenda kuishi kwa majirani baada ya mumewe, Isaya Petro kuezua paa la nyumba waliyokuwa wakiishi na kuhamisha baadhi ya samani za ndani, akimlazimisha kuhama pamoja na watoto wake hao ili aiuze kwa sababu anajifungua watoto wa kike tu.

Nyumba hiyo ambayo Miriam aligoma isiuzwe kwa sababu ni ya familia, ipo katika Mtaa wa Chamoto, Serengeti mkoani Mara.
Tukio hilo lililotokea Alhamisi na Ijumaa iliyopita, limethibitishwa na uongozi wa Kata ya Stendi Kuu huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed akisema Petro ameshakamatwa na atafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu shtaka la kuharibu mali.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, Miriam alisema mumewe alifikia uamuzi wa kuezua paa la nyumba yao baada ya jaribio lake la kwanza la kutaka kuiuza kugonga mwamba kwa kuwa Mahakama ilimtaka aendelee kuihudumia familia yake.

“Baada ya jaribio la kwanza kushindikana, alikuja Alhamis saa tatu usiku na kuniambia lazima auze nyumba na kunitaka niondoke na watoto kwamba ninaweza kuishi kwa mke wake mwingine. Nikamjibu sipo tayari na wala sitaweka saini ya tendo hilo, mume wangu aliapa kwamba lazima tukose wote,” alisema Miriam.

Alisema baada ya malumbano hayo, Petro aliondoka na baada ya muda alirejea akiwa ameshika panga mkononi na kuanza kubomoa mlango.

“Nilipiga kelele huku akinifukuza lakini nikasaidiwa na watoto ndipo baada ya muda majirani walikuja kusaidia. Kuona hivyo mume wangu aliondoka na kuapa lazima afanye kitendo hiki (kunifukuza kwenye nyumba) kwa sababu mimi sina faida namzalia watoto wa kike tu,” alisema. Baada ya tukio hilo alikwenda Polisi na kufungua jalada namba MUG/IR/1230/2018 la kuharibu mali.

Alisema asubuhi ya siku iliyofuata, Petro alifika tena nyumbani hapo na kupanda juu ya paa, kuanza kuezua mabati upande mmoja jambo lililomlazimu kutoa taarifa Serikali ya Mtaa na polisi.

“Pamoja na Polisi kutaarifiwa hawakuweza kufika. Aliendelea kutoa mabati akahamisha vitanda, makochi na vitu vingine aliviharibu. Diwani na watu wengine wakapiga simu kuomba mgambo wakaja wakamkamata na kumpeleka polisi Mugumu na kuwekwa mahabusu,” alisema.
Alidai kuwa lengo la mumewe baada ya kuiuza nyumba hiyo ni kupata fedha za kumjengea mke wake mwingine.

“Kwa muda mrefu amekuwa mkatili na hata watoto wetu haoni kama wana faida yoyote,” alisema Miriam.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Joseph Magoiga alisema Mahakama na Idara ya Ustawi wa Jamii walishatoa uamuzi kuwa nyumba hiyo isiuzwe kwa sababu Miriam ana watoto.

“Kwa mila na desturi za Kikurya nyumba ikishaezuliwa paa, mume na mke hawatakiwi kurudi. Petro alifanya hivyo ili yule mama (mkewe) asirudi na yeye apate nafasi ya kuuza nyumba akimbilie Ngara kwao na mke mdogo wakaishi huko. Kwa sasa mkewe na watoto wanalala kwa majirani,” alisema Magoiga.

Wakizungumza kwa masikitiko watoto wakubwa wa Miriam, wa kwanza mwenye miaka 15 anayesoma kidato cha pili Shule ya Sekondari Mugumu na mwingine miaka kumi na moja wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kambarage, waliomba Serikali iwasaidie kwa kuwa kitendo cha nyumba yao kuezuliwa paa ni ukatili.

Diwani wa kata hiyo, Charles Tunda aliomba sheria ichukue mkondo wake kwa kuwa kitendo hicho ni sawa na kujichukulia sheria mkononi.

“Athari zake ni kubwa kwa familia hasa katika kipindi hiki cha mvua. Hawa watoto na familia yao wataishi wapi?”
Mwita Zakayo ambaye ni jirani na familia hiyo, alisema alimshuhudia Petro akihamisha samani za ndani kupeleka kwa ndugu yake anayeishi jirani na eneo hilo huku akiwaacha watoto wake wakiwa hawana mahali pa kuishi.

“Walitoa taarifa Aprili 5 na 6 lakini hakuna polisi aliyetokea wakati eneo lenyewe lipo mjini kabisa, sasa ingekuwa kijijini sijui ingekuwaje? Ndio maana watu hujichukulia sheria mkononi kwa uzembe huu,” alisema mmoja wa majirani kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Mohamed alisema Petro atafikishwa mahakamani kwa kosa la kuharibu mali.
“Hilo ni kosa la jinai huwezi kuharibu mali kama njia ya kutaka kufukuza familia.

Kama taratibu za kisheria za kuuza zimeshindikana anatakiwa kutii,” alisema.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi huku akisisitiza kwamba, “Mali za familia zinatakiwa kuheshimiwa.”

Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: