Monday, 23 April 2018

Mmoja afariki na wawili kujeruhiwa vibaya kisa ugomvi wa mapenzi


MTU mmoja amefariki na wawili kujeruhiwa vibaya kwa kukatana mapanga mkoani Mara, kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika kijiji cha Kingongo wilayani Serengeti.Kamanda Ndani alimtaja marehemu kuwa ni Kibure Samwel (39) ambaye alichomwa kisu tumboni na kifuani.

Aidha aliwataja majeruhi kuwa ni Nyanga'anyi Waitara (44), ambaye alijeruhiwa mkononi na Munge Samwel (44) aliyejeruhiwa kwenye paja.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Ndani alisema chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa mapenzi ambapo mwamamke (jina limehifadhiwa) alikuwa mke wa Waitara na sasa ameolewa na Munge.

Alisema tangu mwanamke huyo aolewe na Munge kumekuwa na mgogoro baina yao na siku ya tukio walianza kutoleana maneno makali na baadaye kuanza kupigana kwa kutumia mapanga.

Kamanda Ndani alieleza kuwa katika ugomvi huo aliyefariki ni mdogo wa Munge ambaye alipofika kwenye tukio alimkuta kaka yake anashambuliwa na Waitara.

Kamanda Ndani alisema baada ya kuona hivyo, akaamua kuchukua panga ili kumsaidia kaka yake lakini Waitara alimuwahi na kumchoma kisu tumboni na kifuani na kufariki.

"Aliyefariki ni mdogo wake Munge Samwel ambaye katika ugomvi huo alifika kwenye tukio na kukuta kaka yake anashambuliana kwa silaha na Waitara, akaamua kuchukua panga kumsaidia ndipo mtuhumiwa akamchoma tumboni kisha kifuani na kufariki," alisema Kamanda Ndani.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kirenero, Joseph Mwita alisema mgogoro huo ni wa muda mrefu ambapo Waitara alimshutumu Munge kuwa ndiye chanzo cha mgogoro wa ndoa yake na kusababisha mke wake kudai talaka.

Alisema Waitara alikataa kurudishiwa mahari na Munge ili amchukue mke wake kwa madai kuwa ameshazaa naye watoto watatu.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: