WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) imenunua mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo kwa ajili ya viwanja vya Dar es Salaam, Songea, Mwanza na Dodoma.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Atashasta Nditiye, alisema hayo juzi bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Dk. Damas Ndumbaro.

Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji ni kwa nini uwanja wa Songea hauongezwi urefu na kufanyiwa ukarabati ili kutoa huduma zaidi na kuruhusu ndege kutua saa 24.

"Je, ni kwa nini serikali haiweki mashine za ukaguzi wa abiria ili kuondoa adha kwa abiria kukaguliwa mizigo yao kwa kupekuliwa ambapo inadhalilisha na kupoteza muda wao?" alihoji Mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Nditiye alisema tayari mashine hizo zimepelekwa katika viwanja husika kikiwamo cha Songea.

"Hivi sasa mafundi wanaendelea na kazi ya kufunga mashine hizo na tunatarajia kuwa ifikapo katikati ya mwezi huu kazi hiyo itakuwa imekamilika na kuanza kutumika katika viwanja hivyo,"alisema.

Alibainisha kuwa kiwanja cha ndege cha songea ni miongoni mwa viwanja 11 nchini vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP).

Alisema usanifu huo ulikamilika Juni, mwaka jana na ulihusisha usanifu wa miundombinu ya viwanja hivyo kwa ajili ya upanuzi na ukarabati ili kukidhi mahitaji ya viwanja hivyo.

Nditiye alifafanua kuwa hadi sasa wizara yake kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) inaendelea na taratibu za kumpata mkandarasi pamoja na mhandisi mshauri kwa ajili ya kazi za awamu ya kwanza za upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Songea.

Alisema shughuli hizo zitahusisha ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka ndege, barabara za viungo,maegesho ya ndege,kusimika taa na mitambo ya kuongozea ndege hivyo kuruhusu ndege kuruka na kutua kwa saa 24.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: